Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 5:32 am

NEWS : UN KUCHUNGUZA MAUAJI YA ASKARI 15 WA TANZANIA NCHINI KONGO


UN kuchunguza mauaji ya askari 15 wa Tanzania nchini Kongo DR

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema taasisi hiyo ya kimataifa itachunguza mauaji ya wanajeshi 15 wa kulinda amani raia Tanzania waliouawa mapema mwezi uliopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

António Guterres amemteua mwanadiplomasia wa Russia, Dmitry Titov ambaye amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN kuongoza uchunguzi huo.

Kadhalika maafisa wawili wa ngazi za juu wa jeshi la Tanzania pamoja na maafisa wa Umoja wa Mataifa wameteuliwa na UN kwenye jopo la kufanya uchunguzi huo.

Mwezi uliopita, serikali ya Tanzania kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa iliutaka Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi wa kina na wa wazi juu ya mauaji ya askari wake hao, walioshambuliwa na wapiganaji wa kundi la waasi wa ADF la Uganda huko Kongo DR.

JWTZ ikiomboleza mauaji ya askari wenzao Tanzania

Tukio hilo lilitokea Desemba 7, 2017 katika kambi ndogo iliyoko katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu.

Askari waliouawa walikuwa ni sehemu ya askari 3,000 wa timu ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.