Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 9:36 am

NEWS : UMOJA WA MATAIFA WAIKOSOA BURUNDI KWA KUWEKA VITISHO DHIDI YA MAAFISA WAKE

Umoja wa Mataifa waikosoa Burundi kwa kutishia maafisa wakeUmoja wa Mataifa waikosoa Burundi kwa kutishia maafisa wake

Ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeikosoa vikali serikali ya Burundi kwa kuwatishia wataalamu wa uchunguzi wa umoja huo.

Rupert Colville, msemaji wa Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameiandikia barua serikali ya Bujumbura akiitaka iwaonye maafisa wake dhidi ya kutishia maisha ya wajumbe wa Kamisheni ya Uchunguzi ya UN, waliotoa mwito wa kubebeshwa dhima maafisa wa ngazi za juu wa Burundi wanaotuhumiwa kufanya jinai dhidi ya binadamu.

Katika barua hiyo, Colville amesema Burundi kama nchi mwanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa inapaswa kushirikiana na kuheshimu maamuzi ya chombo hicho.

Hivi karibuni, Burundi ilitangaza kuwa haitashirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) katika uchunguzi wa jinai za kivita na ukatili uliofanyika nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Maafisa usalama wa Burundi wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya raia

Novemba 9 mwaka huu, majaji wa mahakama hiyo waliruhusu kuanzishwa uchunguzi kuhusu ukatili na jinai dhidi ya binadamu uliofanywa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2017 dhidi ya raia wa Burundi ndani au nje ya nchi hiyo. Jinai hizo ni pamoja na mauaji, ubakaji, ukatili na mateso yaliyoanza mwaka 2015 baada ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea kiti hicho kwa muhula wa tatu mfululizo.Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Oktoba 26, Burundi ilijiondoa rasmi kwenye Mkataba wa Roma uliounda ICC.