Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 3:40 am

NEWS: UKOSEFU WA ZAHANATI WAWATESA WANANCHI WA KJIJI CHA KITONGA.

KIJIJI cha Kitonga Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, kina zaidi ya miaka 40 kikikabiliwa na changamoto ya kutokuwa na kituo cha huduma za afya.

Kutokana na hali hiyo, wakazi wake wamekuwa wakilazimika kwenda vijiji vya jirani kupata matibabu.

Hayo yalisemwa na mkazi wa kijiji hicho, Rashid Ally, katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalla Ullega.

Ullega ambaye ni mbunge wa Mkuranga, alifanya ziara katika vijiji vya Kiziko na Kitonga katika Kata ya Mwalusembe .

Lengo la Ullega katika ziara ya hiyo ni kukagua miradi ya maendeleo ambayo inasimamiwa na kutekelezwa na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akiwa Kijiji cha Kitonga, Rashid Ally alisema kijiji kilianzishwa mwaka 1977, lakini hakina huduma za afya na hali hiyo inasababisha wanakijiji kufuata huduma za afya katika vijiji vingine.

“Kijiji kina wanakijiji zaidi ya 6,000, kaya 437, lakini zahanati hakuna,” alisema.

Aliongeza kuwa wanamuomba mbunge awatatulie kero hiyo.

Ullega akijibu suala la zahanati alisema wanakijiji wanatakiwa kuonyesha juhudi zao za kuanzisha ujenzi wa zahanati na hatua hiyo itasaidia kupatiwa msaada.

“Kuna vijiji nimetembelea vinakabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini wameweza kuanza ujenzi na kuwa na saruji nami nikachangia ili waweze kufanikiwa kufikia malengo, hivyo nawashauri nanyi muanze kujitoa, ili msaidiwe,” alisema.

Ullega aliwaahidi na kuwahakikishia wananchi hao kuwa atawaunga mkono kwa kuchangia mifuko ya saruji na fedha iwapo nao wataanza kuweka nguvu zao za kujenga zahanati hiyo.