Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 7:53 am

NEWS: TSC YAWAANDIKIA BARUA WALIMU WALIOBAINIKA KUFANYA UDANGANYIFU KATIKA MITIHANI YA DARASA LA 7.

DOM: Tume ya Utumishi ya Walimu(TSC) imeanza kuchukua hatua za awali za kuwaandikia barua za kuwasimamisha kazi walimu wote waliobainika kuhusika kufanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba uliofanyika mwezi septemba mwaka huu.

Kati ya walimu hao waliochukuliwa hatua hiyo wapo walimu 6 wa shule za msingi wilaya ya Chemba mkoani Dodoma ambayo matokeo yake yote yalifutwa,walimu wanne wa shule za msingi zilizopo wilayani Kondoa mkoani Dodoma na walimu wawili wa shule za msingi wilayani Buchosa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo jijini Dodoma katibu wa Tume hiyo Winifrida Rutaindurwa amesema walimu wengine waliohusika wamepewa hati za mashtaka mpaka pale uchunguzi utakapokamilika wa kubaini ushiriki wao katika suala hilo.

Amesema kanuni za TSC za mwaka 2016 zimeelezea kosa la kuvujisha taarifa za siri kinyume na sheria ya Usalama wa Taifa pamoja na adhabu zake ikiwa inajumuisha makosa mbalimbali ikiwemo kufungua bahasha za maswali ya mitihani kabla ya wakati wake na kuonyesha watahiniwa,kuwasaidia majibu au kuwafanyia mtihani na walimu wasiohusika kuonekana katika maeneo ya vyumba vya mitihani siku ya mtihani.

Ametoa rai kwa walimu kuzingatia maadili yao ya kazi na viongozi kutotoa maagizo ambayo utekelezaji wake unakuwa mgumu.

Ametoa onyo pia kwa baadhi ya walimu wenye tabia ya kukiuka maadili yao kazi kwa kutembea na wanafunzi ilhali mwalimu wajibu wake ni kulea wanafunzi kimaadili,kiafya na kielimu.

Mwaka 2017/2018 TSC iliwafungulia mashtaka ya kinidhamu walimu elfu 6,394 yakiwemo makosa ya utoro asilimia 85,kughushi asilimia 2.3,uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi asilimia 2.1,kutotii uongozi asilimia 1.3 na makosa mengineyo aslimia 9.3.