Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 12:49 am

NEWS : TRUMP AANZA SAFARI YA ASIA KWA MASHAKA KIBAO

Trump aanza safari yenye mashaka mengi barani Asia

Trump aanza safari yenye mashaka mengi barani Asia

Rais Donald Trump wa Marekani ameanza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Asia baada ya kusimama kwa muda mfupi katika jimbo la Hawaii.

Safari hiyo ya kuzitembelea nchi tano za Asia ambazo ni Japan, Korea Kusini, China, Vietnam na Ufilipino inahesabiwa kuwa ndefu zaidi kuwahi kufanywa na Rais wa Marekani barani Asia katika kipindi cha robo karne iliyopita. Katika safari hiyo ambayo itaendelea kwa kipindi cha siklu 12, Trump pia atashiriki katika mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Bahari ya Pasifiki (APEC) huko Vietnam na katika kikao cha viongozi wa nchi za Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) kitakachofanyika nchini Ufilipino.

Baadhi ya tathmini na chambuzi zilizotolewa huko Marekani zinasema kuwa, Donald Trump ameanza safari hiyo ya muda mrefu barani Asia kwa shabaha ya kutoroka anga inayotokota nchini kwake hususan mivutano iliyosababishwa na kutiwa nguvuni mkuu wa zamani wa timu yake katika kampeni za uchaguzi na vilevile tukio la kigaidi lililotokea New York na mjadala mkali juu ya muswada wa marekebisho ya kodi.

Wamarekani wanaandamana kupinga sera za Trump

Pamoja na hayo kiongozi huyo wa Marekani atakumbana na mashaka kadhaa akiwa barani Asia. Miongoni mwa matatizo hayo ni jitihada za Washington za kutaka kudhibiti uwezo wa silaha za nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini na kutafuta ufumbuzi wa hitilafu za kibiashara za Marekani na waitifaki na wapinzani wake wenye nguvu kubwa barani Asia.

Trump kukabiliana uso kwa uso na Rais wa China, Xi Jinping

Kuhusu suala la kukabiliana na makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini, kuna aina fulani ya umoja wa kimitazamo kati ya Washington, Tokyo na Seol. Kwa msingi huo maafisa wa serikali ya Marekani wanatarajia kwamba, rais wa nchi hiyo na marais wenzake wa nchi za Japan na Korea Kusini watatuma ujumbe mzito kwa Pyongyang ili Korea Kaskazini itazame upya miradi yake ya makombora na silaha za nyuklia. Hata hivyo inapasa kueleweka kuwa, mashinikizo ya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini yatakuwa butu iwapo Donald Trump hatafikia mapatano muhimu na China, nchi ambayo ataitembelea katika awamu ya tatu ya safari yake ya sasa barani Asia. Wachina licha ya kushirikiana na jamii ya kimataifa katika kuiwekea mashinikizo Pyongyang, lakini hadi sasa wamekataa matakwa ya Marekani ya kukata kikamilifu ushirikiano wao wa kibiashara na kifedha na Korea Kaskazini. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, mazungumzo ya Trump na viongozi wa China kuhusu makombora na silaha za nyuklia za Korea Kaskazini ndiyo yatakayokuwa sehemu ngumu zaidi ya safari ya Donald Trump barani Asia.

Trump ana kibarua kigumu kuhusu makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini

Masuala ya kibiashara pia yanapewa umuhimu mkubwa katika safari ya Trump barani Asia. Sera za kibiashara za Trump zinawatia wasiwasi washirika wa kibiashara wa Marekani barani Asia na hata waitifaki wa Washington kama Japan na Korea Kusini wameweka wazi wasiwasi na masikitiko yao kuhusu tabia ya serikali ya Marekani ya kukiuka majukumu yake. Trump ameahidi kukabiliana na biashara ziada ya nchi kama Japan na China kupitia njia ya kuweka masharti mazito na kuzuia uingizaji wa bidhaa za kigeni nchini Marekani na vilevile kuzuia kupelekwa rasilimali na vitega uchumi vya nchi hiyo katika masoko yenye faida nono zaidi duniani ya mashariki mwa Asia, suala ambalo hapana shaka litawakasirisha sana washirika wa Washington na vilevile mpinzani wake mkubwa wa kiuchumi yaani China.

Inatazamiwa kuwa, hitilafu hizo pia zitadhihiri na kujitokeza katika mukutano wa APEC nchini Vietnam na ule wa ASEAN nchini Ufilipino.