Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 6:49 am

NEWS: TFS YAPEWA SIKU 30 KUMALIZA MGOGORO WA MSITU WA HIFADHI YA MBANGALA

MTWARA: Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga ametoa 30 kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kukaa pamoja na wataalamu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wazee wa maeneo ya Nantona na Mchoti ili kuweza kubaini mipaka halisi katika Msitu wa Hifadhi ya Mbangala ili wananchi hao waweze kujua hatima zao.

Agizo hilo limetolewa wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Njalawa kata ya Mbunguli wilayani Masasi mkoani Mtwara, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi mkoani hapo kwa ajili ya kutatua changamoto za Maliasili, Malikale pamoja na Uendelezaji utalii.

Chanzo cha mgogoro huo ni wananchi wanadai kuwa maeneo ya Nantona na Mchoti waliyokuwa wakitumia kama mashamba yao yamekewa mipaka na TFS kuwa ni sehemu ya Hifadhi ya Msitu.

"Kwa sasa tunasisitiza uhifadhi shirikishi, TFS nawaagiza muiteni mtaalamu kutoka Wizara ya Ardhi ili aje aoneshe mipaka halisi ya maeneo hayo ili mgogoro huo uishe. Alisema Mhe.Hasunga.

Ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi zilizo chini ya Wizara yake kuwashirikisha wananchi na wataalamu wa kusoma ramani wa Wizara ya Ardhi kila wanapotaka kuweka mipaka kwenye maeneo yao.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kanda ya Kusini TFS, Ebrantino Mgiye amesema wananchi walishirikishwa kikamilifu wakati wa uwekaji wa mipaka hiyo.