Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 7:55 am

NEWS: TARURA WAWASHUSHIA LAWAMA WANANCHI KWA KUHARIBU MIUNDOMBINU YA BARABARA.

BAHI DOM: Wakala wa Barabara mijini na vijijini(TARURA),wamelalamikia kitendo cha wananchi kupitisha mifugo katika barabara wanazotengeneza na kuharibu miundombinu hiyo hali inayosababisha kutodumu kwa muda mrefu.

Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa Tarula, Samwel Muganizi wakati akitoa taarifa za hali ya barabara katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2017/18 kilichofanyikawilaya ya Bahi Mkoani Dodoma.

Mugamizi Amesema, Tarura wanapata changamoto kubwa kutokana na wananchi kupitisha mifugo barabarani jambo ambalo limekuwa likichangia kwa kasi kuharibu miundombinu ya barabara.

Mbali na hayo amewaomba madiwani kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi kuacha kuleta athari katika miundombinu ya barabara.

Akiendelea ameongeza kwa kuwataka madiwani kutoa elimu kwa wananchi na kuwaelekeza kupitisha mifugo yao kwenye barabara za pembeni ili waweze kutunza miundombinu hiyo.

"Tatizo ni kubwa tunatengeneza barabara lakini zinaharibika lakini wanabaki wakilaumiwa Tarura lakini tatizo ni mifugo, tunaomba madiwani mtusaidie sana," amesema.

Kuhusu hali ya barabara amesema, zinahitaji matengenezo makubwa hivyo wanafanya kulingana na bajeti.

Amesema, wameanza na maeneo korofi ambapo pia wamepata wafadhili tayari wamepita nao katika maeneo yote na wamerudi nchini marekani wanawasubiri warudi wakiwa wamechagua maeneo ya waliyoamua kusaidia kufadhili katika matengenezo ya barabara.

Wakati akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Danford Chisomi, amewataka Tarura kutoa taarifa kwa madiwani kuhusu barabara zinazotengenezwa ili wajue na kutoa ushauri maana wao ndio wawakilishi wa wananchi.

Amesema, kumekuwa na muingiliano na baadhi ya sekta mfano, sekta ya ardhi hivyo wanapotaka kupima viwanja wahakikishe wanawashirikisha Tarura ili nao waweze kuweka barabara jambo ambalo pia litaongeza thamani katika viwanja hivyo.

Mwenyekiti huyo pia amesema , jambo hilo litasaidia kupanga mji vizuri na kufanya mambo yao kwa tija kwa manufaa ya halmashauri na wananchi kwa ujumla.