- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: TANZANIA KUONGOZA UZALISHAJI UMEME AFRIKA MASHARIKI
Dar es Salaam: Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ametanabaisha kuwa mradi huu wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge ambao umetiwa saini leo ukikamilika utakuwa mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki kwa kuzalisha megawati 2,115.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumatano Desemba 15, 2018 Ikulu Dar es Salaam wakati wa utiaji saini wa ujenzi wa mradi huo katika Bonde la Mto Rufiji mkoani Pwani, Dk Kalemani amesema bwawa linalofuata kwa kuzalisha umeme mwingi ni la Bujagari nchini Uganda, likitarajiwa kuzalisha megawati 300 tu.
“Afrika Mashariki sasa ni wa kwanza tukiwa na megawati 2,115. Bwawa lililokuwa likiongoza kabla yetu ni lile la Bujagari la Uganda bado linajengwa na lina megawati 300,”amesema Dk Kalemani.
Amesema kwa Afrika, Tanzania itakuwa ya nne na kwamba nchi inayoongoza kwa kuwa na mabwawa makubwa ni Ethiopia, akibainisha kuwa bwawa lake la Renaissance linaloendelea kujengwa litazalisha megawati 6,450 na ujenzi wake utakamilika 2022.
“La pili lipo Mambira Nigeria linazalisha megawati 3,050, la tatu liko Ethiopia ambalo ni Shaika likizalisha megawati 2,160. Bwawa la nne ndiyo la kwako Rais (John) Magufuli (akimaanisha Stiegler’s Gorge),” amesema.
“Bwawa la tano liko Misri (Aswan Dam) la megawati 2,100 na la sita liko Angola la Rauka linalozalisha megawati 2,066. Hongera sana rais.”
Mbali na Afrika, Dk Kalemani amesema Tanzania ni kati ya nchi 60 zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme, akisema jumla yapo 70.
Amesema bwawa kubwa kuliko yote liko China likizalisha megawati 22,500, la pili nchini Brazil (megawati 14,000) na jingine China (megawati 13,860).
“Malengo yetu ni kufikisha megawati 5,000 mwaka 2020 na megawati 10,000 mwaka 2025 kwa hiyo kukamilika kwa mradi huu ni matumaini yetu kwamba pamoja na kuwa na umeme, lakini umeme wa uchumi wa viwanda mradi huu ni injini ya uchumi wetu,” amesema.
Amesema mradi huo unatekelezwa na makandarasi kutoka Misri wakifanya kazi kubwa nne; kujenga kuta mbili kubwa zenye urefu wa mita 1,025 na kimo cha mita 131, kujenga bwawa kubwa la kutunza maji lenye urefu wa kilomita 100 na upana kilomita 25 na uwezo wa kubeba mita za ujazo bilioni 35.2.
“Kazi ya tatu ni kujenga mtambo wa kuzalisha umeme, utakuwa na mitambo tisa na kila mmoja utazalisha megawati 235 na jumla yake zitakuwa megawati 2,115,” amesema Dk Kalemani na kuongeza:
“Kazi ya nne ni kujenga kituo cha kufua umeme mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda.”