- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: TANZANIA KIDEDEA KWA UTAWALA BORA AFRIKA
SERIKALI za Tanzania, Rwanda na Kenya zimezitoa kimasomaso nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kufanya vizuri kwenye masuala ya utawala bora miongoni mwa nchi 54 barani Afrika, huku Tanzania ikishika nafasi ya kwanza katika vipengele vitatu.
Kwa kuzingatia ripoti ya mwaka huu ya utafiti, uliofanywa na Taasisi ya Mo Ibrahim, Tanzania imekuwa ya kwanza kwenye vipengele vitatu vya usalama wa taifa kwa kupata alama 100 kwenye kila kipengele.
Tanzania pia imefanya vizuri kwa kuwa ya kwanza Afrika kwenye kipengele cha ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kupata alama 75.0, ya tatu kwa kuzuia ubaguzi alama 50.0, ya nne kwa usawa wa jinsia sehemu za kazi alama 50.0, na ya tisa kwa ushiriki wa wanawake kwenye siasa alama 56.7.
Ripoti hiyo iitwayo IIAG ya utafiti uliofanywa mwaka jana, inaonesha kuwa kwa ujumla, Tanzania imeshika nafasi ya 11 Afrika kwenye masuala ya usalama wa taifa kwa kupata alama 91.1. IIAG inafanya utafiti kwenye vigezo mbalimbali kikiwemo cha usalama na utawala wa sheria, ushirikishwaji na haki za binadamu, fursa endelevu za kiuchumi na maendeleo ya binadamu.
Ripoti hiyo ina lengo la kuunga mkono utawala bora na uongozi barani Afrika. Kwenye eneo la usalama wa taifa, Tanzania imepata alama 100 kwa ushiriki wa serikali kwenye migogoro ya silaha, alama 100 kipengele cha kuyahama makazi ndani ya nchi, alama 100 kwa wakimbizi wa kisiasa, na pia imefanya vizuri kwenye kipengele cha kuvuka mipaka kwa sababu ya hofu.
Kwa kuzingatia ripoti hiyo ya kila mwaka, kwa ujumla Tanzania imeshika nafasi ya 17 kwa utawala bora barani Afrika kwa kupata alama 57.5. Ripoti ya IIAG imekuwa ikichapishwa tangu mwaka 2007. Kwenye utawala wa sheria, Tanzania imekuwa ya 23 Afrika kwa kupata alama 56.3, na kwenye uwajibikaji imekuwa ya 15 alama 45.5.
Katika uwajibikaji Tanzania imeshika nafasi ya 17 barani Afrika kwa uwajibikaji maofisa wa Serikali, ya nne kwa huduma kwa umma kwa intaneti ikipata alama 77.5, ya sita kwa uchunguzi masuala ya rushwa alama 55.6, na ya 13 kwa uwajibikaji na uwazi kwenye sekta ya umma alama 66.1.
Tanzania pia imefanya vizuri kwa kuwa ya 10 Afrika usalama wa mtu mmoja mmoja. Kwenye eneo hilo imepata alama 58.9, imeshika nafasi ya 14 kwa migogoro ya kisiasa, na ya 11 kwa uvunjaji sheria.
Imekuwa ya 16 kwenye ushirikishwaji na haki za binadamu kwa kupata alama 61.5, na imekuwa ya sita kwa uhalali wa michakato ya kisiasa kwa kupata alama 77.8. Tanzania imekuwa ya 10 kwa utoaji wa haki barani Afrika kwa kupata alama 58.2, na ya 11 kwenye masuala ya jinsia kwa alama 68.9. Kwa kuzingatia ripoti hiyo, kwa mwaka wa tano mfululizo, Mauritius imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kwa utawala bora miongoni mwa nchi 53 za Afrika.
Afrika ina nchi 54 lakini kwenye ripoti hiyo ya matokeo ya sera kwenye utawala bora, Sudan na Sudan Kusini zimetambuliwa kuwa ni nchi moja. Kwa kuzingatia ripoti hiyo, Mauritius imeongoza kwa kupata alama 81.4.
Kwa kuzingatia ripoti hiyo, Rwanda imekuwa ya tisa kwa utawala bora barani Afrika. Nchi nyingine kwenye 10 bora na alama zao ni Seychelles (73.4), Botswana (72.7), Cape Verde (72.2), Namibia (71.2), Afrika Kusini (70.1), Tunisia (65.5), Ghana (65.0), Rwanda (63.9), na Senegal (61.6).
Kwenye nchi nyingine wanachama wa EAC, Kenya imekuwa ya 13 kwa utawala bora Afrika kwa kupata alama 59.3, Uganda ya 19 alama 56.5, Burundi imekuwa ya 44 alama 39.9 na Sudan Kusini ya 53 alama 20.2.
Rwanda imezishinda nchi nyingine za Afrika kwenye vigezo vitano kati ya 14. Vigezo hivyo na alama ilizopata kwenye mabano ni kama ifuatavyo: Mazingira ya biashara (83.0), sekta vijijini (83.6), hali bora (79.2), uwajibikaji (72.1) na usawa wa jinsia (87.3).
Kwa mujibu wa ripoti, nchi hiyo imekuwa ya nne kwenye kipengele cha afya kwa kupata alama 86.7 na imekuwa ya tano Afrika kwa usalama wa mtu mmoja mmoja. Tangu kuanza kutolewa kwa ripoti hiyo mwaka 2007, Rwanda imekuwa ikifanya vizuri.
Kwa mfano, mwaka 2010 ilikuwa ya 31 kati ya nchi 53, na mwaka 2014 ikawa ya 11 kati ya nchi 52 kwa kupata alama 60.4. Mwaka 2013 ilikuwa ya 15. Kwenye ripoti ya mwaka huu, Somalia imeshika mkia kwa utawala bora, Afrika Kusini ina wastani wa juu wa alama, na Afrika ya Kati ina wastani wa chini.
Kwa mwaka huu, taasisi ya Mo Ibrahim imetoa tuzo kwa Rais wa zamani wa Cape Verde, Pedro Verona Pires. Tuzo hiyo inatolewa kwa kiongozi wa zamani wa serikali aliyekuwa amechaguliwa kidemokrasia, ambaye alikaa madarakani kwa kuzingatia ukomo wa muda uliowekwa kwenye Katiba ya nchi, aliyeondoka madaraka miaka mitatu iliyopita, na alifanya vizuri akiwa madarakani.
Mshindi wa tuzo anapata zawadi ya Dola za Marekani milioni tano na Dola za Marekani 200,000 (Sh milioni 440,000 za Tanzania) kila mwaka kwa maisha yake yote.