Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 4:03 pm

NEWS: TALGWU ''HATUKUBALIANI KABISA NA KANUNI HIZI ZINAZOMLIPA MSTAAFU''.


DODOMA: Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Suleiman Kikingo amesema (TALGWU) haikubaliani kabisa na kanuni zinazotumiwa na kikokotoo cha mafao ya pesheni yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii kumlipa mstaafu na kudai kuwa ni kiwango kidogo sana cha mafao ukilinganisha na kanuni zilizokuwepo awali.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma wakati wa tamko la chama hicho kuhusu mkanganyiko wa kikokotoo cha mafao hayo amesema kuwa wanaunga mkono msimamo wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Kuwa kanuni hizo na sheria mpya ya mifuko ya hifadhi ya jamii kuanza kutumika kumezua taharuki kubwa kwa wanachama wao.

“Tunakubaliana na TUCTA kuwa hii ni kanuni kandamizi kwa wastaafu ambayo imepokelewa na wafanyakazi kwa mtazamo hasi na imeshusha ari,morali na ufanisi wa kazi kwa wanachama wetu” amesema Kikingo.


Pia ameitaka Serikali kurudi kwenye meza ya pamoja katika kujadiliana na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kwa dhumuni la kupatia suluhisho la suala la Kikokotoo cha mafao ya kustaafu kwa maslahi ya Wafanyakazi.

“Wito wetu kwa Waziri mwenye dhamana pamoja na serikali kwa ujumla ni kuwa wakumbuke na kutambua mchango wa wafanyakazi wa nchi yetu na walione jambo hili katika mtazamo chanya”amesisitiza

Amesema kuwa kilio hicho cha wafanyakazi ambao ndio walipaji wa kodi na wanaochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi siyo cha kupuuzwa.

Wakati huo huo amewaasa wanachama wa TALGWU kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu ambacho viongozi wa vyama vya wafanyakazi kupitia TUCTA wanashughulikia suala hilo na waendelee kuwa na imani na chama chao.

“Tunaamini serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ni sikivu na tunategemea suala hili litapatiwa ufumbuzi”

Hata hivyo amesema kuwa wafanyakazi wa Serikali za Mitaa ndio watumishi wa Umma wanaolipwa mishahara midogo.

“Kwa hali hiyo ndiyo kundi kubwa linaloathirika na kanuni hii mpya kwa kumlipa mastaafu mafao yake kwa asilimia 25 kama malipo ya mkupuo na kubakiza asilimia 75 ambazo serikali imepanga kuwalipa wastaafu kama pensheni ya kila mwezi”alisema Kikingo.

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TALGWU taifa na mwakilishi wa wafanyakazi mkoa wa Kagera Dk. David Mapuda amesema kuwa ni wakati wa Serikali kukaa meza moja kumaliza mzozo huo na iwapo hawatakuwa tayari kufanya hivyo wafanyakazi ambao ni wapigakura wao watapewa mrejesho na kuona nini kifanyike.