Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 5:43 pm

NEWS: TAASISI ZATAKIWA KUWA CHACHU YA KUSIMAMIA MAADILI NCHINI.

DODOMA: Katibu Tawala msaidizi wa Mkoa wa Dodoma Emanuel Kuboja amezitaka Taasisi zote za umma, sekta binafsi na makundi mbalimbali katika jamii kuwa chachu ya kuliwezeshaTaifa letu kutekeleza na kusimamia uwajibikaji, uadifu, haki za binadamu, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa ili kufikia uchumi wa kati na waviwanda.


Ametoa agizo hilo leo mjini Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati wa ufunguzi wa kutoa huduma kwa umma katika kuadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa.

Kaboja amesema serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dk John Magufuli , imeazimia kwa dhati kabisa kufikisha nchi ya Tanzania katika uchumi wa kati na wa viwanda.

Mbali na hayo amesema madhumuni ya Tanzania kushiriki katika kuadhimisha siku ya maadili na haki za Binadamu ni kuliwezesha Taifa letu kuudhirishia ulimwengu dhamira yake ya dhati ya kusimamia kwa vitendo dhana ya misingi ya uadilifu, haki za binadamu, utawala bora, uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.

Pia ameongeza kuwa madhumuni mengine ni pamoja na kuimarisha nidamu katika utumishi wa umma na kuongeza kasi ya maendeleo kwa Taifa letu.

Awali akizungumza kamishina wa maadili ya viongozi wa umma Jaji Harold Nsekela amesema ili kufanikisha adhima ya serikali ya awamu ya tano ya kufikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ni lazima kujenga maadili kwani ndio msingi muhimu katika utendaji hasa Taasisi zote za umma na kwa mwananchi mmoja mmoja.

Tarehe 9 Desemba kila mwaka, nchi wanachama wa umoja wa mataifa (UN) huadhimisha siku ya kimataifa ya kuzuia na kupambana na rushwa (International Anti_Corruption Day) ambayo kwa Tanzania huanzimishwa Desemba 10 na huitwa siku ya maadili.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ''Wajibika piga vita rushwa , zingatia maadili, haki za binadamu na utawala bora kuelekea uchumi wa kati''.