- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: SPIKA AKASIRISHWA NA MANENO YA CAG, AMTAKA YEYE NA MDEE KUHOJIWA NA BUNGE
Dodoma: Spika wa Bunge Job Ndugai amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge siku ya Januari 21, 2019 kwa hiari kwa ajili ya kuhojiwa, vinginevyo atapelekwa kwa pingu.
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo mchana Januari 7, 2019 alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake akisema Profesa Assad amelidhalilisha Bunge.
Ndugai amesema CAG akiwa nje ya Tanzania wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili alisema Bunge la Tanzania kuwa ni dhaifu.
"Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji, huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana," amesema Ndugai.
Ndugai amesema kitendo hicho kimemkasirisha kwani hakutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu uhuru.
Mbali na CAG, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye ameitwa mbele ya kamati hiyo siku inayofuata yaani Januari 22, 2019.
Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.
CAG alijibu: "Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.
"Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa."
Akiendelea kufafanua jibu lake, CAG Assad alisema: "Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua."