Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:40 pm

NEWS: SIMBACHAWENE AZITAKA TAASISI ZA FEDHA KUPUNGUZA RIBA KWENYE MIKOPO.

Taasisi za fedha nchini zimetakiwa kupunguza riba kwenye mikopo inayotolewa kwa vikundi vidogo vidogo ili viweze kujikwamua kiuchumi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti George Simbachawene alipokuwa akifungua Mkutano wa 20 wa Chama cha kuweka na kukopa cha Walimu Mpwapwa, mjini humo.


Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe, alisema kwasasa kinachoonekana kwenye taasisi hizo ni kutoa mikopo yenye riba kubwa jambo linalosababisha ziweze kufa.


“Mkopo wenye riba kubwa hauna urafiki na masikini bali una lengo la kudidimiza wanyonge, hizi taasisi zinazotoa mikopo zinatoa kwa riba kubwa jambo linalosababisha zingine kufa, kufilisiwa mali zao,”alisema.


Alieleza kuwa lengo la vyama vya ushirika au vya kuweka na kukopa ni kuwasaidia wanyonge ambao wanakuwa wameunganisha nguvu kupambana na umasikini.


Mwenyekiti huyo alisema wilaya ya Mpwapwa inakadiliwa kuwa na walimu zaidi ya 1500 kama wangeingia kwenye chama chao wote kusingekuwa na haja ya kukopa kwenye taasisi za fedha bali wangetumia fedha za chama chao kusaidiana.


Awali, Mwenyekiti wa chama hicho Piniel Loilole alisema kwa mwaka 2018 kiasi cha Sh.Milioni 82.15 kilitolewa kwa wanachama kama mikopo ya dharura na ya kawaida.


Naye, Meneja wa chama hicho, Joackim Mokiwa alisema changamoto kubwa inayowakabili kwa mwaka huu ni hasara ya Sh.Milioni 6.68 iliyotokana na baadhi ya watumishi kugundulika kuwa na vyeti feki hivyo kukosa sifa ya kuwa wanachama huku wakiwa tayari wamechukua mikopo.