Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:35 am

NEWS: SHERIA YA MADAWA YA KULEVYA YATUA BUNGE

DODOMA: Mkutano wa tisa wa Bunge la 11 unaanza vikao vyake leo mjini Dodoma huku muswada wa marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya wa mwaka 2017 ukitarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza.


Muswada huo ni miongoni mwa miswada minne iliyopo katika ratiba ya shughuli za Bunge zitakazoanza leo hadi Novemba 17.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai aliitaja miswada mingine itakayojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa mwaka 2017.

Aidha, Kagaigai alisema miswada mingine ni Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 4 wa mwaka 2017.

Kadhalika, katibu huyo alisema wabunge watajadili na kupitisha mapendekezo ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali katika mwaka wa fedha unaofuata wa 2018/19.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge ya 94(1), katika mkutano wa Oktoba-Novemba kwa kila mwaka, Bunge litakaa kama kamati ya Mipango kwa siku zisizopungua tano ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(C) ya Katiba kwa kujadili na kuishauri serikali kuhusu mapendekezo hayo.

Mbali na hilo, alisema kutakuwapo na kiapo cha Mbunge wa kuteuliwa, Janeth Masaburi ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli na pia kutakuwa na maswali 125 ya kawaida na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.