Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 6:33 pm

NEWS: SERIKALI YASEMA TATIZO LA UTAPIAMLO LIMEPUNGUA NCHINI.

DODOMA: Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Pawaga, amefungua mkutano wa kwanza wa Maafisa Lishe wa Mikoa nchini ambao unahusisha Wataalam wa kada hiyo waliopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe ambao una lengo la kuboresha lishe katika Jamii.

Akifungua kikao hicho mjini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu Mohamed Pawaga, amesema tatizo la utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano nchini limepungua kwa kiasi kikubwa. “takwimu za Utafiti wa Afya na Demografia Nchini za mwaka 2015/16 zimebaini kupungua kwa viwango vya Kitaifa vya utapiamlo hasa kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 kwa viashiria vya Udumavu, Ukondefu na Uzito pungufu ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka 2010.

Aidha amesema, kiwango cha Udumavu Kitaifa kimepungua kutoka asilimia 42.8 hadi 34.7, Ukondefu kutoka asilimia 4.8 hadi 3.0 na Uzito Pungufu kutoka asilimia 16 hadi 13, jambo ambalo amesema ni jitihada kati ya Serikali na Wadau katika masuala ya lishe.

Amewataka washiriki hao kufanya kazi stahili na kutoa taarifa za kila robo ya mwaka wa fedha kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ili wafahamu kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa shughuli za Lishe kulingana na Mkataba watakaosaini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI mwishoni mwa mwezi Desemba, 2017.

Amewataka washiriki kuufanyia kazi Mpango Jumuishi wa Lishe wa Taifa – 2016/2021 ambao umejikita kwenye maeneo matatu ya Mpango wa pamoja, Usimamizi wa pamoja na Uratibu wa pamoja wa shughuli za Lishe kati ya Serikali na wadau lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa uwajibikaji, uwazi na ufanisi unakuwepo ili kujitathmini ni eneo lipi linafanywa vizuri na lipi linahitaji kuboreshwa ili kupunguza utapiamlo katika jamii.

Kwa upande wake Dkt. Rasheed Maftah ambaye ni Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI, amesema kuwa, Mkutano wa kazi huo una lengo la kujadili mbinu za utendaji kazi na kuwapa Maafisa Lishe maelekezo muhimu kuhusu utendaji kazi ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuleta matokeo bora katika kuimarisha hali ya Lishe nchini na hasa katika kutekeleza “Mpango Jumuishi wa Lishe wa Taifa, 2016 – 2017”

Bwana Stephen Motambi Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema kuwa kikao kazi hicho kina lengo la kuwajengea uwezo Maafisa Lishe wa Mikoa ili kuweza kutekeleza shughuli za Lishe katika mikoa yao kwani kwa hivi sasa nchini hali ya udumavu bado si nzuri sana mbayo ni watoto 34 kati ya 100 wanakabiliwa na utapiamlo unaotokana na lishe duni hivyo Washiriki watajadili suala la lishe kama changamoto mojawapo ili kupunguza idadi ya watoto wadumavu ambao wanaliongezea gharama Taifa kwa matibabu yao.

Naye msoma risala ya washiriki, Rehema Napegwa amesema ili kufanikisha utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe wa Julai 2015/16 hadi Juni 2020/21 na kuleta matokeo yaliokusudiwa ni mapendekezo yetu kuboresha na kutatua changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mkakati wa lishe wa Taifa wa mwaka 2011/12 hadi 2015/16, ikiwa ni pamoja na kuongeze bajeti yake katika kutekeleza afua za lishe na kutoa vibali vya ajira ili Mikoa na Halmashauri ziweze kuajiri watalaamu wa lishe