Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 4:45 pm

News: Serikali yaruhusu sekta binafsi kulipa mshahara zaidi ya kima cha chini.


Serikali imesema sekta binafsi wanaruhusiwa kuwalipa watumishi wake zaidi ya kiwango cha kima cha chini cha mshahara pale ambapo wanaona kufanya hivyo itaongeza motisha kwa wafanyakazi wao.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, amesema bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Septemba 11, akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), aliyeuliza katika kipindi cha na maswali na majibu bungeni endapo serikali haioni haja ya kuboresha mishahara yake na kuzielekeza sekta binafsi kulipa mishahara inayoendana na hali ya maisha.


Akijibu hilo Mavunde amesema, serikali imeweka utaratibu kwa waajiri na wafanyakazi katika sekta binafsi, kujadiliana na kufunga mikataba ya hali bora mahali pa kazi kwa lengo la kuboresha maslahi yao ikiwamo mshahara na stahiki nyingine.


“Kupitia utaratibu huu, sekta binafsi wanaruhusiwa kulipa zaidi ya kima cha chini ili kuwafanya wafanye kazi kwa bidii na kujituma kwa lengo la kuzalisha mali au katika ktoa huduma.


“Hata hivyo, pia Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7, ya mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mwaka 2015, imeanzisha Bodi ya Mishahara ya sekta binafsi ambayo ina jukumu la kufanya utafiti kwa kuzingatia hali halisi ya gharama za maisha na masuala mengine ya kiuchumi na kupendekeza kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi,” amesema.


Pamoja na mambo mengine, Mavunde amesema serikali iko katika hatua za mwisho za kuiwezesha bodi hiyo kufanya utafiti kuhakikisha utafiti huo unakidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu zinazokubalika nchini na viwango vya kimataifa.