Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 1:38 am

NEWS: SERIKALI YAJIPANGA KUJENGA VITUO KUCHUNGUZA WATAKAOBAINIKA NA DALILI ZA UGONJWA WA EBOLA.

DOM: Mkurugenzi wa huduma za udhibiti wa ubora kutoka wizara ya afya Dk, Mohammed Mohammed amesema serikali imejipanga kujenga vituo vya kuhifadhia na kuwachunguza watakaobainika kuwa na dalili za Ugonjwa wa ebola katika mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa Dk, Mohammed amesema kuwa licha ya kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini lakini serikali ni lazima ichukue tahadhari kwa ajili ya kujikinga na virusi vya ebola.

Amesema kuwa serikali inaanza kujenga vituo hivyo katika mikoa hiyo kutokana na kuwa raia wengi wa kigeni wanaosafiri hupitia viwanja vya ndege katika mikoa hiyo.

Amesema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha inajenga vituo katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kwa sasa kuna tumu za wataalamu ambao wamepelekwa katika maeneo ya mipakani kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za kinga wizara ya afya Dk.Leonard Subi amewatahadharisha walaji wa nyama pori hususani sokwe kuchukua tahadhari ya kutokula nyama hiyo ili kuepuka kupata ugonjwa wa Ebola.

Amesema kuwa ugonjwa wa Ebola umeibuka tena katika nchi ya Kidomokradia ya Congo ambapo hadi sasa wagonjwa 30 wamegundulika kufariki kwa ugonjwa huo, huku akitoa tadhadhari wale wanaokula nyamapori aina ya sokwe na wal wanakumbatia pamoja na kubusu maiti kuachana na mila na desturi za aina hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi kitenge cha mazingira kutoka Wizara ya Afya Dk, Halid Massa amesema kuwa mipaka ndio geti la kupitishia ugonjwa hio hivyo ni lazima geti hilo kudhibitiwa kwa kuwa na wataalamu wa kutosha katika mipaka hiyo.