Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 2:32 pm

NEWS: SERIKALI YAFUTA ADA NA TOZO ZILIZOKUWA ZIKILALAMIKIWA NA WAWEKEZAJI.

JIJINI DOM: Serikali imefuta ada na tozo zaidi ya tano ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wawekezaji kwa muda mrefu huku ikisisitiza kuendelea kusimamia afya na usalama mahala pa kazi.

Pia, katika kuondoa mwingiliano wa kero za ukaguzi ambapo zimekuwa zikipunguza ufanisi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulamavu, Jenista Mhagama amesema kuanzia sasa idara zote za serikali ambazo zinawajibu wa kukagua zitafanya ukaguzi jumuishi.

Waziri huyo ameyabainisha hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mchango wa Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi( OSHA) katika kujenga uchumi wa viwanda.

Ametaja tozo hizo zilizofutwa au kufanyiwa marekebisho kuwa ni pamoja na ada ya fomu ya usajili, ada ya usajili wa maeneo ya kazi kwa kuzingatia ukubwa wa eneo, faini inayohusiana na vifaa vya kuzima moto.

Nyingine ni ada ya leseni ya kukidhi matakwa ya sheria ya usalama na afya mahali pa kazi na tozo ya siku ya ushauri wa kitaalamu kwa usalama na afya kwa kuzingatia idadi ya wafanyakazi.

Awali amesema Machi mwaka huu, Rais John Magufuli kwa utaratibu wake mzuri alikutana na wadau wa sekta binafsi ikiwa ni pamoja na TPSF ili kuzungumza namna ya kujenga mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara nchini na kuongeza kasi ya uwekezaji hasa katika viwanda.

Vilevile, kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika miradi ya ujenzi wa uchumi nchini pamoja na mambo mengi yaliyojadiliwa na kuazimiwa ilikuwa ni pamoja na kufanya mapitio ya sheria ya Afya na Usalama mahala pa kazi Na, 5 ya mwaka 2003 na kanuni zake.

Amefafanua kuwa katika kutekeleza jambo hilo OSHA imefanya mambo mbalimbali ambapo ni pamoja na kutengeneza program maalum ya utoaji elimu kwa wadau kuhusu takwa la kisheria la kulinda afya za wafanyakazi nchini mahala pa kazi katika kanda mbalimbali.

“Msisitizo huu pia ni matakwa ya malengo ya umoja wa mataifa na utekelezaji wa vipengele vilivyomo kwenye lengo namba 8 la malengo ya maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa ambalo ni kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wote ifikapo mwaka 2030 na kukomesha ajira mbaya za watoto ifikapo 2025,”

Waziri huyo ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2017/18 jumla ya ajali 755 ziliripotiwa kwa mujibu wa sheria ambapo sita kati ya hizo zilizababisha vifo, 749 majeruhi.

Aidha, sekta ya usalishaji iliongoza kwa kuwa na asilimia 87 ya ajali zote ambapo sekta ya madini ilikuwa na asilimia saba, ujenzi asilimia nne na sekta zilizobaki ikiwa ni asilimia mbili.

Akizungumzia Sheria hiyo, Mkuu wa kitengo cha Sheria OSHA, Joyce Bupe amesema kwa kiasi kikubwa sheria hiyo itawagusa watu wote wanaojishughulisha na kazi mbalimbali nchini.

Amesema pia ipo kwenye jinai na kwamba mtu akifanya kosa anaweza kupewa faini au kufungwa.