Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:32 am

NEWS: SERIKALI YA AWAMU 5 YAJISIFU KUJENGA VITUO 67 VYA AFYA

Dar es salaam: Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbas amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli imeongeza pakubwa ujenzi wa Hospitali za Wilaya na vituo vya afya nchini ambapo kwa miaka mitatu pekee jumla ya vituo hivyo 67 vimejengwa ukilinganisha na 77 vilivyojengwa miaka 53 iliyopita tangu uhuru.

Akizungumza katika semina ya Waandishi kupitia Klabu ya waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar Es Salaam (DDCPC) iliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF iliyokuwa na lengo la kujengeana uwezo ili umma wa watanzania waweze kunufaika zaidi katika huduma za Afya Nchini, Dkt Abbasi amesema ipo haja kwa waandishi wa habari hao kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.

Dkt Abbasi amesema hatua hiyo ya Serikali ya ujenzi wa kasi wa hospitali na vituo vya afya inalenga kuimarisha afya za watanzania ambapo hivi sasa idadi kubwa ya watanzania inatumia huduma za bima ya afya ya Taifa NHIF idadi ambayo awali ilikuwa milioni 9.9 mwaka 2015 mpaka kufikia zaidi ya milioni 16 Mwaka huu wa 2018.

“Unajua hata sisi waandishi wa habari tunayo haki ya kupongeza,pale unapoandika changamoto na zikafanyiwa kazi ni muhimu kupongeza pia sio kukosoa tu, juhudi za Serikali ya awamu ya tano kwa kipindi kifupi tu makubwa yamefanyika ukilinganisha na kipindi kingine chochote” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa Serikali.