Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 6:52 pm

NEWS: SERIKALI KUREKEBISHA SHERIA YA TLS

BUNGENI DOM: Serikali imewasilisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba 2 wa mwaka 2018 unaopendekeza kurekebisha sheria ya Chama Cha Wanasheria Tanganyika kwa kuweka vigezo vitakavyotumika kupata wajumbe wa baraza.

Akiwasilisha mabadiliko ya muswada huo sept 7 bungeni jijini hapa waziri wa katiba na sheria Profesa Palamagamba Kabudi amesema marekebisho hayo ni katika sura namba 307 kwa kuweka vigezo na taratibu za kufuatwa wakati wa utungaji wa kanuni zinazosimamia chama hicho.

Profesa Kabudi amesema muswada huo pia unalenga kufanya marekebisho ya sheria ya urejeshwaji wa mali zitokanazo na uhalifu sura ya 256 yanayolenga kuimarisha mfumo wa kisheria wa kuhakikisha wahalifu hawafaidiki kutokana na mali walizozipata kwa njia ya uhalifu.

Akiwasilisha maoni na ushauri wa kamati ya bunge ya Katiba na Sheria kwa niaba ya mwenyekiti,mjumbe wa kamati hiyo dokta Damas Ndumbaro ameshauri kuhuisha sheria ya TLS ambayo haijafanyiwa maboresho tangu ilipoanza kutumika mwaka 1955 hali inayosababisha chama kushindwa kuendana na zama zilizopo.

Wakichangia muswada huo mbunge wa Tabora Mjini Emmanuel Mwakasaka ameipongeza serikali kwa kupeleka marekebisho hayo na kutoa angalizo katika sura ya 256 inayohusiana na urejeshwaji wa mali zitokanazo na uhalifu huku mbunge wa viti maalum Salome makamba akisema mabadiliko hayo yanamlenga mtu jambo ambalo profesa Kabudi amelisisitiza kuwa mabadiliko ya sheria hizo hayamlengi mtu yoyote.

Sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho katika muswada huo ni sheria ya kabidhi mkuu,sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai,urejeshwaji wa wahalifu,sheria ya tafsiri ya sheria,ukomo,tume ya kurekebisha sheria Tanzania na mashirikiano katika masuala ya jinai.

Sheria nyingine ni sheria ya ofisi ya Taifa ya mashtaka,utekelezaji wa majukumu ya ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali,sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa,sheria ya kuzuia ugaidi,sheria ya mapato ya uhalifu a sheria ya chama cha wanasheria Tanganyika.

Lengo la Marekebisho hayo linatajwa kuwa ni kuimarisha utendaji wa taasisi za wizara ya katiba na shria kwa kuondoa mwingiliano wa majukumu ya kitaasisi,kuhuisha miundo ya baadhi ya taasisi ikiwemo ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ili kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi zetu.’

Muswada huo unatarajiwa kupitishwa siku ya jumatatu kutokana na leo akidi ya wabunge kutotimia.