Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 6:37 pm

NEWS: SERIKALI KUFANYA MAPITIO YA MIRADI YA MAJI KUANZIA MWAKANI.

ARUSHA: Serikali imewaagiza Wahandisi wa maji kuhakikisha wanasimamia miradi ya sekta ya maji nchini inayozingatia thamani ya shilingi na yenye kuleta tija kwa Watanzania.

Akiongea katika ziara yake mkoani Arusha katika wilaya ya Longido Mhe. Joseph George Kakunda, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, amesema kumekuwepo na ufujaji wa fedha za katika Miradi ya maji nchini na mara nyingi imekuwa sio endelevu na yenye kuleta hasara kubwa kwa Taifa.

“Wahandisi hakikisheni mnasimamia utekelezaji wa miradi ya maji kwa thamani ya shilingi, wale wote wanaojenga miradi hiyo muwasimamie vizuri, fedha tunazozikopa hakikisheni mnazitumia vizuri, acheni kupokea rushwa, nataka kuona Wahandisi wanajenga mradi kwa maslai ya watu wa Longido ili kuondoa kero za maji, zingatieni taratibu, kanuni na sheria ili tupate tunachostahili”

Mhe. Kakunda amewataka Watendaji na Wahandisi kufanya mapitio ya miradi ya maji nchini ili kuona miradi iliyotekelezwa kwa halali na pia ili iliyotekelezwa kwa wizi ionekane. “haiwezekani tangu tuanzishe Programu ya Maji Vijijini tumekwisha tumia zaidi ya shilingi trilioni 1.6lakini bado kila sehemu kuna shida ya majikwa nini kila mradi una maisha yake kama miaka 10, 15, 20, 25 hili haliwezekani, hatuwezi kwenda namna hiyo, mimi nitapendekekeza tufanya mapitio ya miradi yote ya maji iliyojengwa hasa kuanzia mwaka 2008. Kwanini watu wa kawaida wanajenga mradi mkubwa kutoka kwenye chanzo hadi hapa”

Akiwa kijijini Elondeka, Mhe. Kakunda amepongeza hatua zilizofikiwa za Mradi wa maji unaotekelezwa na Mradi wa Tabia nchi (DCFP)ambao umegharimu kidogo cha fedha shilingi milioni 36 na kushauri wananchi kuulinda siku zote. Pia alikagua mradi wa maji unaotekelezwa na Halmashauri ya wilaya Longido ambao bado haujakamilika.

Akisoma taarifa ya mradi mbelel ya Mheshimiwa Naibu Waziri Kakunda, Mtesigwa Missana ambaye ni Afisa Tarafa Longido amesema kuongezeka kwa kutotabilika kwa tabia ya hali ya hewa yanazidisha changamoto kama vile kubadilisha mtindo wa maisha ya wananchi.

Aidha, Mhe. Kakunda amewaasa wananchi kuulinda mradi wao waliouchagua wenyewe, “toeni ushirikiano kwa mradi huu kwa sababu mmeuchagua wenyewe, lindeni sana mradi huu ili uweze kuhudumia ninyi wenyewe na mifugo, mradi huu una faida kwenu ninyi, mifugo na wanyama wa porini”