Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 5:35 pm

NEWS: SERIKALI HAITAWALIPA WATUMISHI WALIOFUKUZWA KWA KUWA NA VYETI FEKI .

Serikali imesema haitawalipa watumishi waliofukuzwa kazi kwa kuwa na vyeti feki kutokana na udanganyifu huo.


Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Aida Khenani bungeni jijini Dodoma leo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika amesema serikali haijapanga kumlipa mtumishi yeyote ambaye mkataba wake ni feki.


Akiuliza swali hilo, Aida amesema kabla ya kupunguzwa kwa watumishi hao waliodaiwa kuwa na vyeti feki, serikali ilikuwa na vyeti feki na hadi sasa kuna upungufu wa watumishi wa kiasi gani.


“Serikali ya Tanzania inathamini zaid vyeti kuliko taaluma, kuna wengine walikuwa wamebakisha mwaka mmoja tu ili wastaafu, je, serikali ina mpango gani wa kuwalipa watumishi hao,” amesema.


Mkuchika akijibu hilo amesema; “Mwajiri alikuajiri akijua vyeti ulivyompelekea ni sahihi, kitendo cha kumdanganya kinafuta mkataba wenu na serikali haijapanga kuwalipa watumishi wa aina hiyo,”

Katika swali lake la msingi, Aida alitaka kujua mkakati wa serikali kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti feki ambapo Waziri Mkuchika alijibu serikali imeshatoa kibali cha kuajiri watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo la lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti.