Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:37 am

NEWS: SAKATA LA KUZUIA MJADALA WA TUNDU LISSU WAZUA MZOZO WAKILI WA CHADEMA AMSHUKIA IGP SIRRO

Wakili wa CHADEMA, John Malya amefunguka na kuzungumzia juu ya kauli ya IGP Sirro kuhusu kuzuia wanasiasa kuzungumzia sakata la Lissu na kusema IGP hana mamlaka hayo kuzuia wananchi kuzungumzia jambo lolote na kufanya hivyo ni kuvunja sheria.


John Malya amesema hayo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Kinondoni na kusema kuwa Sirro anapaswa kukaa kimya sasa na kuendelea na uchunguzi wa sakata hilo ila hana mamlaka ya kuzuia wananchi wasitoe mawazo yao wala kuzungumzia jambo fulani.


"Kamanda Sirro alinukuliwa akiwa Mbeya anasema amepiga marufuku wanasiasa kujadili masuala yanayomuhusu Tundu Lissu na kujadili watu ambao labda wanasadikiwa au wanashukiwa kwamba wameshiriki jaribio la kumuuwa Lissu.Nimefikiri ni muhimu kumkumbusha IGP Sirro kuwa yeye ni kamanda wa Polisi na si kamanda wa raia hana mamlaka ya kutoa amri wananchi wajadili nini na nini wasijadili mamlaka hayo hana na nitatoa ufafanuzi.


"Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki na fursa ya wananchi kutoa maoni, kuzungumza mawazo yao na kubadilishana habari, ndiyo ibara ambayo inawapa wananchi na nyinyi waandishi wa habari uhuru wa kufanya kazi zenu katika nchi hii pamoja na sheria zingine lakini ibara ya 18 ndiyo msingi haswa wa kwanini wananchi wana uhuru wa kupashana habari na kuwa na uhuru wa mawazo" alisema Malya


Malya alisema kuwa IGP naye anaongozwa na sheria na kanuni mbalimbali na kusema katika hizo sheria na kanuni ambazo zinamuongoza IGP katika kutenda kazi zake za kila siku hakuna sehemu ambapo anapewa mamlaka ya kuzuia wananchi kujadili jambo fulani na kusema anaweza kufanya hivyo kwa askari lakini si kwa wananchi.


"Kamanda Sirro anaongozwa na sheria kadhaa lakini kubwa anaongozwa na sheria ya jeshi la polisi na huduma saidizi, na msaafu anaotumia unaitwa 'Police General Order' (PGO). Kwenye jeshi la polisi hii ni sheria maarufu sana wao wenyewe wanaijua ndiyo inasema IGP anamuamuru nani na nani hawezi kumuamuru sasa huko anaweza kuwaamuru askari wake wasijadili au wasifanye kitu fulani, lakini kusema yeye amuru raia mamlaka hayo hana kwenye sheria wala kanuni" alisisitiza Malya


Aidha Malya anasema kuwa wananchi wanasubiri kusikia kauli ya IGP Sirro kuhusu upelelezi wa jambo hilo, au kusikia watu ambao wamekamatwa na kupelekwa mahakamani lakini si kuwazuia watu wasijadili shambulio alilolipata Tundu Lissu na kudai kuendelea kufanya hivyo ndiko kunapelekea hata wananchi pamoja na wao kuwa na mashaka na jeshi la polisi katika kufanya uchunguzi wa jambo hilo.


"Wakati huu ambapo wanasiasa, wapiga kura wanajadili juu ya hali ya Tundu Lissu yeye Sirro anapaswa kunyamaza, hapa yeye ndiyo anapaswa kunyamaza na siyo wanasiasa, yeye anyamaze afanye kazi ya upelelezi kitu cha pili tunachotaka kusikia amepeleka watu mahakamani, hivyo kufanya hicho anachokifanya anazidi kutufanya kukosa imani zaidi na jeshi la polisi" alisisitiza Malya