Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:37 am

NEWS: RC MGHWIRA AAMPA SIKU 3 MKURUGENZI MOSHI KUJIELEZA

Moshi: Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Anna Mghwira atoa siku tatu za kujieleza kwa maandishi kwa mkurugenzi wa manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi kushindwa kusimamia taratibu za uendeshaji wa masoko na usafi katika manispaa hiyo.

"Nataka ndani ya siku tatu mkurugenzi ajieleze kwa nini ameshindwa kusimamia usafi, kuweka utaratibu mzuri wa masoko kiasi cha wafanyabiashara kuweka bidhaa hovyo wakati tumeshatoa maagizo siku nyingi,” amesema Mghwira.

Akizungumza leo Jumatatu Januari 7, 2019 Mghwira amesema sifa za manispaa hiyo kwa usafi zimepotea kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri na wanasiasa.

Mkuu huyo wa mkoa leo amefanya ziara ya kushtukiza katika soko la Mbuyuni na kushuhudia wafanyabiashara wakiwa wamepanga vyakula chini kinyume na taratibu huku uchafu ukiwa umezagaa pembezoni mwa barabara.

Amesema kushindwa kusimamia usafi kumesababisha manispaa hiyo kushuka katika nafasi yake ya kwanza iliyokuwa ikishikilia katika usafi kitaifa, kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu.

Pia, amemtaka meya wa manispaa hiyo, Raymond Mboya kuacha kuchanganya siasa na utendaji na kubainisha kuwa usafi hauna chama.

“Hali ya usafi katika masoko yetu ni mbaya mno, cha kushangaza meya wa manispaa anawaeleza wafanyabiashara warudishe bidhaa barabarani wakati tumeshatoa maagizo bidhaa zisionekane pembezoni mwa barabara kwani zinafanya mji kuwa na mwonekano mbaya,” amesema Mghwira