Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:39 am

NEWS: RC MBEYA AAGIZA UWONGOZI SOKO LA MBEYA KUWEKWA NDANI

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, Amevunja uongozi wa soko la Sido la Jijini Mbeya Huku akiagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata viongozi wote wanaohusika na soko hilo ili kujibu tuhuma mbali mbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kutafuna fedha za Rambirambi za Shiling milioni 10 zilizotolewa na Naibu Spika Dkt Tulia Ackson kwa wauzaji waliounguliwa na maduka yao,

pia viongozi hao wa soko wanatuhumiwa kushawishi wafanyabiashara wa soko hilo kutolipa kodi, hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato tangu mwaka 2007 lilipoungua soko la Mwanjelwa.

"Uongozi wa soko hili nimeuvunja kuanzia dakika hii na ninamwagiza RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) awakamate viongozi hao, awaweke ndani na baadaye ndipo tuzungumze nao waeleze mahali ziliko fedha hizo," alisema Chalamila

Pia aliagiza wafanyabiashara wote wanaotumia soko la Sido kuhakikisha wanapata leseni na kulipa kodi ya pango la chumba cha biashara kabla ya kesho na kuonya kuwa yeyote atakayekaidi baada ya muda huo kupita, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Chalamila alisema wafanyabiashara wote wanatakiwa kutia saini mkataba maalumu wa umiliki wa chumba cha biashara sokoni hapo kwa kuwa vibanda vya soko hilo vimejengwa kwenye eneo la serikali.

Alisema kila mfanyabiashara baada ya kutia saini mkataba, atatakiwa kulipa Sh. 50,000 kwa ajili ya pango ambapo nusu ya fedha hiyo itachukuliwa na mtu aliyejenga kibanda na nusu itakuwa mali ya serikali kama ushuru wa pango.