Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 12:29 am

NEWS: RC ATEMBELEA DAMPO LA KISASA MANISPAA YA DODOMA, ASEMA DODOMA LAZIMA IWE SAFI ZAIDI.

DODOMA: Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge amesema Mji wa Dodoma hauna sababu ya kuwa mchafu kwa sababu Manispaa ya Dodoma imetekeleza mradi wa ujenzi wa dampo la kisasa na litakalodumu kwa miaka mingi ijayo.

Aliyasema hayo baada ya kutembelea dampo la kisasa la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu takribani umbali wa kilometa 12 kutoka katikati ya Mji wa Dodoma.

Katika ziara hiyo fupi, Mkuu huyo wa Mkoa alioongozana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rehema Madenge pamoja na Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji wa Manispaa hiyo Dickson Kimaro aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.

Awali mara baada ya kuwasili katika eneo la dampo, Mheshimiwa Mahenge alielezwa jinsi Dampo hilo la kisasa linavyofanya kazi na Mhandisi wa Mazingira wa Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida, aliyemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, dampo hilo linatumia teknolojia ya kuzika taka ardhini (Sanitary Landfill) ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wakazi wa maeneo ya karibu na dampo.

Mhandisi Faida alimjulisha Mheshimiwa Mahenge kuwa, dampo hilo tayari limeanza kufanya kazi mapema mwaka huu, na limejengwa kwa fedha za mradi wa Kuimarisha Miji ya Kimkakati Tanzania (TSCP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kuratibiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.