Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:53 pm

NEWS : RAIS WA ZIMBABWE AANZA KUSHUGHULIKA NA MAFISADI WA FEDHA ZA UMMA

Rais Mnangagwa wa Zimbabwe atoa muhula wa miezi mitatu kwa walioiba fedha za umma kuzirejesha

Rais Mnangagwa wa Zimbabwe atoa muhula wa miezi mitatu kwa walioiba fedha za umma kuzirejesha

Rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ametoa muhula wa miezi mitatu kwa wale wote waliopora fedha za umma na kuzificha nje ya nchi kuzirejesha.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, Mnangagwa amesema muhula huo ukimalizika Februari mwakani, serikali itawakamata na kuwafikisha mahakamani wale wote ambao hawatakuwa wametii amri hiyo.

Hayo yanajiri wakati ambao aliyekuwa waziri wa fedha wa Zimbabwe, Ignatius Chombo ambaye alikuwa amekamatwa na jeshi baada ya kuchukua mamlaka, alifikishwa mahakamani Ijumaa iliyopita akikabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Kwa mujibu wa wakili wake, waziri huyo wa zamani wa fedha wa Zimbabwe anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka wakati alipokuwa waziri wa serikali za mitaa.

Ignatius Chombo ni miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali ya Zimbabwe waliokamatwa baada ya Robert Mugabe kuzuiliwa nyumbani kwake mnamo tarehe 14 Novemba.

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe

Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefutwa kazi na Robert Mugabe wiki chache zilizopita siku ya Ijumaa aliapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, huku akiahidi kulijenga upya taifa hilo linalokabiliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi.

Sherehe za kumuapisha Mnangagwa zilifanyika katika Uwanja wa Taifa wa Michezo mjini Harare, uliokuwa umefurika makumi ya maelfu ya wananchi wanaosema kuwa nchi yao inashuhudia mwamko mpya.

Jumanne iliyopita, Mugabe ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 37 alisalimu amri na kukubali kujiuzulu, kufutia mashinikizo ya kila upande ya kumtaka aachie madaraka.

Emmerson Mnangagwa ataiongoza Zimbabwe hadi Septemba mwaka ujao 2018, wakati ambapo uchaguzi wa rais utafanyika