Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:37 am

NEWS : RAIS MUGABE AMTIMUA KAZI MAKAMU WAKE

Rais Mugabe wa Zimbabwe amfuta kazi makamu wake

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amempiga kalamu nyekundu makamu wake Emmerson Mnangagwa, kutokana na kile kilichotajwa kama ukosefu wa uaminifu kwa rais na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Hayo yalitangazwa jana Jumatatu na Waziri wa Habari wa nchi hiyo Simmon Khaya-Moyo kwa niaba ya Mugabe mjini Harare na kuongeza kuwa, Emmerson Mnangagwa ameonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kama Makamu wa Rais na pia ameonyesha kutokuwa na uaminifu na heshima hususan kwa kiongozi wa taifa.

Rais Mugabe wa Zimbabwe amfuta kazi makamu wake

Makamu wake aliyemtimua

Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 amekuwa akionekana kama mmoja wa wanasiasa waliotarajiwa kumrithi Rais Mugabe, kufutwa kwake kazi kunaonekana ni njia ya kumuondolea kizuizi mke wa rais Robert Mugabe, Grace Mugabe, aweze kurithi mikoba ya mumewe.

Siku ya Jumapili Grace Mugabe alitoa wito wa kutaka mumewe amfute kazi Mnangagwa kwa tuhuma za kuibua migawanyiko na mifarakano ndani ya chama tawala ZANU-PF.

Emmerson Mnangagwa na Pelekezela Mphoko ni mamakamu wa Rais wa Robert Mugabe serikalini na ndani ya chama tawala, lakini Mnangagwa ndiye anayeelekea zaidi kuwa mrithi wa Mugabe tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wa umakamu wa rais mwaka 2014.

Grace Mugabe

Mnangagwa, ambaye anajulikana kwa lakabu ya Mamba katika lugha ya Kishona aliteuliwa kuwa makamu wa rais baada ya Mugabe kumtimua Joyce Majuru aliyeshikilia cheo hicho kwa muda wa miaka 10.