Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 6:37 pm

NEWS: RAIS MAGUFULI AMWAGA SABABU ZA KUMTUMBUA BOSI WA TAKUKURU

MARA: Rais, John Magufuli, amesema sababu za kumtumbua Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola, ni kutokana na kushindwa kushughulikia jalada lililomfikia mezani kwake na madhambi mengine ya nyuma.

Rais Magufuli alitoa sababu hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime, mkoani Mara ikiwa ni siku moja tangu amwondoe kwenye nafasi hiyo na kumteua kuwa balozi.


Nafasi ya Mlowola ambaye ni Kamishna wa Polisi, imechukuliwa na kamishna mwingine wa jeshi hilo, Diwani Athumani, ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.


Akizungumza na wananchi waliokuwa wamefurika kwenye mkutano huo, Rais Magufuli alisema alikwenda Musoma, mkoani Mara na kukuta mtu aliyeinunua hoteli ya Musoma haiendelezi na kila kandarasi anayopewa haiendelezi.


Alisema hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipita na kutoa maagizo Takukuru walishughulikie tatizo hilo hilo la mnunuzi wa hoteli ya Musoma lakini hakuna kilichofanyika.


“Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara alilishughulikia, akalishughulikia na kulipeleka Makao Makuu ya Takukuru na kuweka mapendekezo yake yote. Makao makuu tangu Aprili hadi mwezi huu hawajalishughulikia.


"Nikaona Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru akae pembeni akafanye kazi nyingine.Nikaangalia na madhambi mengine yakajitokeza nikasema kazi ya kushughulikia rushwa haiwezi,” alisema.


“Nilikaa usiku nafikiria hadi kichwa kikauma, ilipofika saa 11 alfajiri nikafanya kazi. Muda huo ndipo ilitumwa taarifa ya Ikulu kuwa uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru umetenguliwa,”alisema.


Aliongeza kuwa: “Nataka kuwaeleza kuwa watu wangu ninaowateua mshughulikie shida za wanyonge. Ambaye hawezi kufanya hivyo aandike barua ya kuacha kazi. Huwezi kazi lakini mshahara unalipwa. Usafiri unao wananchi maskini kama hawa huwashughulikii wakati wangu hili haliwezekani,” alisisitiza.


Rais Magufuli alimtangazia msamaha Mkuu wa Wilaya ambaye alishindwa kushughulikia tatizo la mama mwenye ulemavu wa macho kuwa, amemsamehe siku hiyo lakini akirudia mara ya pili hatamsamehe.


Akizungumzia kuhusu mwanamke huyo mwenye ulemavu wa macho, Rais Magufuli alisema alikwenda katika kijiji kimoja na kumkuta mwanamke huyo ambaye amedhulumiwa mazao yake na tajiri mmoja mwenye zaidi ya ng’ombe 3,000.


Alisema mama huyo alikuwa anahangaika kila siku na wakati mwingine alikuwa anaanguka kwenye mitaro kwa sababu haoni.


“Amekwenda hadi mahakamani, amekwenda hadi kwa Mkuu wa Wilaya ambaye anamamlaka makubwa lakini hakufanya hivyo na ameendelea kulalamika mpaka nilipofika mimi,” alisema


Aliongeza kuwa: “Nimeumia mno kwamba Watanzania hatumuogopi hata Mungu nilitamani kumfukuza Mkuu wa Wilaya leo, Roho wa Bwana akaniambia tunatakiwa kusamehe saba mara sabini na mimi huwa sijali natumbua tu.”


Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Madini na Mkuu wa Mkoa Mara wamhoji mtu aliyetajwa kwa jina moja la King’anya ambaye ndiye aliyesaini mkataba wa Mfuko wa Fedha wa North Mara (NMRF) ambao fedha zake hazijulikani zipo wapi.


“Palikuwa na malipo ya vijiji kati ya vitano au sita ambavyo viliingia mkataba na mgodi tangu ukiitwa North Mara kabda haijaja kampuni ya Acacia,” alisema.


Alisema vijiji hivyo viliingia mkataba kwamba vingekuwa vinalipwa fedha ndipo ukafungulia mfuko huo lakini akaja mtu mjanja akauanzisha ili ziingizwe humo.


Alisema fedha hizo zimeingizwa kwenye mfuko na zilivyokuwa nyingi ukasimamishwa hivyo Acacia hawawezi kuingiza fedha humo na licha ya hali hiyo viongozi wa serikali wapo lakini hawajafanya chochote.


“Huyu King’anya ndiye anayetakiwa atuambie mfuko una kiasi gani. Waziri wa Madini na Mkuu wa Mkoa mshughulikie suala hili, mumuite King’anya mjue huo mradi una kiasi gani mumueleze huyo King’anya ni kiasi gani cha fedha ambacho hakijalipwa,” alisema.


Rais alisema fedha hizo zingekuwepo hata wangetaka maji ya bilioni tano zingetosha kwa sababu vile vijiji vilikubali.


“Nilitegemea Mbunge, diwani na watendaji wengine Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa wangeshughulikia suala la mfuko huu na kujua fedha hizi zimekwenda wapi na Acacia inatakiwa kulipa kiasi gani lakini hawayashughulikii haya na hawajui mfuko una shilingi ngapi,” alisema.


Alisema mfuko huo umeshikiliwa na matapeli na viongozi kuanzia ngazi ya chini hawajui una kiasi gani.


Diwani wa eneo hilo alipohojiwa na Rais kuhusu fedha za mfuko huo alisema hadi sasa hawajui ni shilingi ngapi zipo na kumtaja King’anya kuwa ndiye anayefanya mahesabu kwa kushirikiana na Acacia.


Rais Magufuli alisema anataka kupata taarifa za fedha hizo zilizopo tangu mfuko ulivyoanza, zilizotumika na zilizobaki.


“Kama hamjui King’anya ndiye mtia saini, wanaofaidika ni wengine ambao ndio watia saini, wananchi hawafaidiki ni sawa na kufuga ng’ombe maziwa wanywe wengine,” alisema.


Rais Magufuli alisema anataka kuijenga Tanzania ili wazulumaji, majizi wote washughulikiwe na ndiyo maana alianza kwa kuwaondoa watumishi hewa, mafisadi wakubwa kwa kuwapeleka mahakamani.


Alisema wote waliosaini katika mkataba huo akiwamo King’anya lazima watoe maelezo fedha za Nyamongo ziko wapi.


Magufuli alisema wapo baadhi ya wananchi ambao wanatakiwa kulipwa fidia ya nyumba na mashamba yao yaliyofanyiwa tathmini lakini baadhi wanategesha ili nao walipwe.


“Tatizo lililopo Nyamongo wajuaji ni wengi maarifa mengi kupoteza njia wamekuja watu wakafanya tathmini wakaja wengine wanategesha, niwaambie wanaotegesha hakuna atakayelipwa, tegesha hata kwenye maji hutalipwa,” alisema.


Alisema orodha ya watu wanaostahili kulipwa fidia ipo na hao wanaotegesha ndio wanaowacheleweshea wanaostahili kulipwa.


Rais Magufuli alisema kuwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi eneo hilo alikuwa hafai ndiyo maana alitolewa.


“Nataka kuwaeleza ukweli nayafahamu ya hapa, mkoa wa Mara umejaa migogoro kila ukifika kuna migogoro, nimefika pale kwenye daraja Nyasurura nimekuta mama amedhurumiwa ni kipofu, akaenda kwa viongozi wote wanamzungusha mpaka amekwenda kwa Mkuu wa Wilaya (DC).


“Nilitamani leo nifukuze DC lakini ana bahati sana. Sitaki watu wanyanyaswe, mimi ni Rais wa wananchi wanyonge na mimi nimetoka familia maskini,”alisema na kuongeza:


“Niwaombe wananchi muendelee kushirikiana na serikali na nyinyi mkubali kusikiliza maelekezo yanayotolewa na serikali,” alisema Katika ziara hiyo, Mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Ingwe, Monica Dunde, alimgusa Rais Magufuli baada ya kupewa nafasi na kueleza changamoto za shule yao zilizosabababisha, atoe fedha taslimu Sh. milioni tano 5 na viongozi wengine kuchangia.


Fedha zilizotolewa ahadi na taslimu ni zaidi ya shilingi milioni 18 ambazo zitakwenda kutatua changamoto za shule hiyo ikiwemo upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa, vitabu, vitanda na mabweni.