Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 9:41 pm

NEWS: RAIS MAGUFULI AAGIZA UONGOZI WA CWT KUHAKIKI MADENI YA WALIMU.

DODOMA: Rais dokta John Magufuli ametoa agizo kwa viongozi wa Chama Cha walimu mkoa na wilaya kuhakiki madeni ya walimu yaliyopo ili wawe na uhakika na uhalali wa madeni hayo.

Akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho Taifa leo mjini Dodoma dokta MAGUFULI amesema deni lililopo kwa sasa ni shilingi bilioni 25 lakini kila kiongozi ahakiki uhalali wa deni hilo na aweke saini yake ili kuyathibitisha.

Akizungumzia benki ya walimu dokta MAGUFULI amesema benki hiyo imekuwa ikisuasua na kuweka wazi kuwa kuna dosari nyingi kulingana na taarifa za benki kuu ya Tanzania BOT ambayo ndio msimamizi mkuu wa benki hapa nchini.

Aidha ameitaka ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI kuangalia upya mgao wa walimu kwa kuwa kwa sasa walimu wengi wamekuwa wakipangiwa katika shule za mijini kuliko Vijijini hali inayosababisha upungufu wa walimu maeneo ya vijijini.

Akizungumzia uchaguzi wa CWT Rais MAGUFULI amesema ni lazima Chama hicho kuhakikisha kuwa kinachagua viongozi ambao watakipeleka chama mbele.

Awali Kaimu Rais wa CWT LEAH ULAYA amesema CWT inaungana na serikali katika vita inayoendelea dhidi ya rushwa na ufisadi na kusisitiza kuwa walimu wapo pamoja naye na kutoa ombi kwa serikali kuwalipa malimbikizo ya madeni yao yanayofikia shilingi bilioni 25.