Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:24 am

NEWS: POLISI WAELEZEA JINSI WATUMISHI 7 WALIOFARIKI KWEYE AJALI

Dodoma: Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Murotto amesema ajali iliyopoteza maisha ya watu saba na kujeruhi wengine watatu wilayani Kongwa jijini Dodoma leo usiku Novemba 3, 2018 imesababishwa na lori lililokuwa limeegeshwa barabarani.

Katika ajali hiyo magari mawili ya ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) yaligongana uso kwa uso baada ya moja ya gari hilo kuhama njia kutokana na kuligonga lori hilo nyuma.

Amesema gari la ofisi ya CAG lilikuwa likitokea Dodoma likiwa na abiria saba na gari la PSSSF lilikuwa na abiria watatu na lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma.

“Chanzo cha ajali ni lori lenye namba za usajili T161 CCB lenye tela namba T152 CCB ambalo lilikuwa limeharibika eneo la barabara,” amesema.

“Gari moja la Serikali liligonga lori hilo nyuma na kupoteza mwelekeo na kugongana uso kwa uso na gari jingine,” amesema.

Amesema abiria na dereva waliokuwa katika gari la CAG wamefariki dunia wakati watatu waliokuwa katika gari la PSSSF wakijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Amesema mwili mmoja umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na miili mingine sita katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa.