Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 12:36 pm

NEWS: PINGAMIZI LA SCORPION LATUPWA.

Mahakama ya Wilaya ya Ilala imetupilia mbali pingamizi la kutopokea maelezo, lililowekwa na upande wa utetezi kwenye kesi ndogo ndani ya ile ya msingi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, inayomhusu Salum Njwete maarufu Scorpion (34).


Scorpion anakabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi kwa kumtoboa macho, Said Mrisho.


Mahakama ilifikia uamuzi huo baada ya upande wa utetezi kudai Scorpion alishurutishwa kutoa maelezo kwa nguvu, ikiwamo kupigwa na kuteswa katika Kituo cha Polisi Buguruni.


Akisoma uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi, Flora Haule alisema mahakama imetupilia mbali pingamizi hilo baada ya kubaini utetezi huo ni kinyume na hoja ya pingamizi lililowekwa awali.


Hakimu Haule alisema kwamba maelezo ya mshtakiwa yanatia shaka kutokana na kutofautiana.


Alisema maelezo ya awali ni kwamba alilazimishwa kutoa maelezo huku akipigwa na kuteswa, lakini mengine anadai aliambiwa aandike ili aachiwe ndio maana alifanya hivyo. Baada ya kutoa uamuzi huo, Koplo Bryghton wa Kituo cha Polisi Buguruni aliendelea na ushahidi.


Scorpion anadaiwa Septemba 6 mwaka jana saa nne usiku, maeneo ya Buguruni, aliiba vitu mbalimbali vya Mrisho vyenye thamani ya Sh474,000 na kwamba, kabla na baada ya kutekeleza uhalifu huo, alimchoma Mrisho sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo machoni, tumboni na mabegani.


Hakimu Haule aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 20.