Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:31 pm

NEWS : NYUMBA ZA IBADA KUBOMOLEWA KIMARA

Bomomoa Bomoa Kuhamia Kwenye Makanisa, Misikiti Kimara Kesho

Bomomoa Bomoa Kuhamia Kwenye Makanisa, Misikiti Kimara Kesho

Nyumba za ibada 24 zinatarajiwa kubomolewa kesho na Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro inayoanzia Kimara hadi Kiluvya.

Ubomoaji wa nyumba hizo za ibada ni mwendelezo wa uboamoaji wa nyumba takribani 1300 za wakazi wa maeneo hayo zinazodaiwa kujengwa ndani ya mita 121.5 ya barabara hiyo.

Nyumba zaidi ya 1000 zimebomolewa mpaka sasa hali inayosababisha baadhi ya wananchi kulala nje kutokana na kukosa makazi .

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu Mhandisi wa Tanroads Kimara ambaye anasimamia

ubomoaji huo ,Jonson Rutechula amesema kesho watakuwa na kazi maalum ya kubomoa nyumba za ibada tu.

“Tumewaambia viongozi wa misikiti na makanisa, waondoe vitu kesho tunakuja kubomoa.Tutabomoa makanisa 14 na misikiti 10 kuanzia eneo la Kimara hadi Kiluvya”amesema

Amesema shughuli ya ubomoaji wa nyumba imekamilika kwa asilimia kubwa ,zimesalia nyumba za ibada tu.”Kama unavyoona karibu ubomoaji wa nyumba za makazi umekamilika tulibakiza nyumba za ibada”amesema

Ameongeza kwamba “Kesho tutabomoa makanisa 14 na misikiti 10 kuanzia eneo la Kimara hadi Kiluvya na tutaanza kazi hiyo asubuhi”amesema Rutechula.

Hata hivyo mwandishi wetu alitembelea Kanisa la Mtakatifu Maria Parokia ya Kimara na kukuta baadhi ya waumini wakitoa vyombo nje na walipoulizwa baadhi ya viongozi waliokuwepo kanisani hapo walikataa kuzungumza .

“Sisi siyo wasemaji, kama unataka habari njoo kesho na kamera zako uchukue matukio lakini pia mtafute Paroko yeye atakwambia nini kinaendelea maana sisi si wasemaji”amesema mmoja wa waumini hao