Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:45 pm

NEWS: '' NI VIZURI TUFIKE MAHALI TUKAJITAMBUA''NDUGAI.

DODOMA: Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wabunge wanatakiwa kupigwa msasa katika suala la maadili kutokana na wananchi wengi kulalamika kuhusu maadili yao, huku akimuomba Kamishna wa Maadili, kuangalia uwezekano wa watunga sheria hao kula kiapo cha uadilifu kama ilivyo kwa watumishi wa umma.

Aidha, wabunge kwa upande wao, wamekuwa na maoni tofauti kuhusu suala hilo la maadili baadhi yao wakihoji manufaa ya kujaza fomu za maadili kila mwaka, lakini hawaoni hatua zikichukuliwa kwa wanaokiuka sheria hiyo, na wengine wakihojiwa baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kwa uadilifu kupandishwa vyeo.

Spika Ndugai na wabunge hao walizungumza hayo jana mjini hapa wakati wa semina ya maadili na udhibiti wa rushwa kwa wabunge iliyoandaliwa na Mtandao wa Wabunge Wanaopambana na Rushwa (APNAC) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Spika Ndugai alisema wabunge wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wamekuwa hawana maadili hivyo akaomba wabunge wapigwe msasa katika eneo hilo.

“Tutakubaliana na waheshimiwa wabunge katika eneo ambalo tunatakiwa kupigwa brashi ni katika eneo la maadili kwani tumenukuliwa na vyombo vya habari na wananchi wametulalamikia kwamba baadhi hatuna maadili,” alisema Spika Ndugai. Alimuomba Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold Nsekela kuangalia uwezekano wa wabunge kula kiapo cha maadili pindi wanapoapishwa.

“Waheshimiwa wabunge tunapoapishana bado hatuna kiapo, napenda kushauri kama kuna umuhimu hili liwepo. Tunapaswa kujua ni namna gani tunaishi katika jamii, maadili yatusaidie katika uongozi wetu,” aliongeza Spika Ndugai. Katika mchango wake, Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy (CCM) alihoji kuwa wamekuwa wakijaza fomu za maadili, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kwa wanaokiuka. “Baadhi ya viongozi walikula pesa na wakarudisha sasa hawa ninyi viongozi wa Maadili mmechukua hatua gani kwa hao viongozi nashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema nyinyi mnasimamia maadili ya viongozi na kila mwaka mnajaza fomu, na viongozi wa nchi hii wana majengo ya ajabu na wanajaza uongo. Mfano, EPA wengine wamerudisha fedha wengine hawajarejesha, wanatanua tu na wengine wapo ndani kwa ushahidi,” alieleza mbunge huyo machachari. “Sasa ninyi kama viongozi mnachukua hatua gani kwa hawa watu ambao wana majumba hayalingani na mishahara yao kila siku tunajaza tu fomu.

Mimi ni mbunge miaka saba kila mwaka najaza tu fomu sioni hatua zozote, mimi nalikataa hili.” Wabunge wengine wakiwamo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walitaka kupata ufafanuzi kutoka kwa Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Nsekela ni kwa nini baadhi ya viongozi wakiwemo wakuu wa wilaya wanaokiuka kanuni za maadili, lakini wamekuwa wakipandishwa vyeo.

Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema) alihoji, “Kama Mwenyekiti wa Maadili hapa katikati kulitokea purukushani nyingi tu, lakini wengine tulikuwa hatuamini, lakini huyo aliyekuwa akituhumiwa kwa rushwa ambaye ni kiongozi katika serikali amesema hadharani na kwenye vyombo vya habari nadhani hata wewe unajua kwa sababu imezunguka sana.

Hamuoni kama tunadanganyana katika mambo ambayo yana uhalisia.” Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema) alisema: “Tunaomba sana wewe Mheshimiwa Jaji siyo nyie mnaangalia maadili kwa watu wadogo wadogo muangalie na kwa hawa watu wakubwa ambao wanafanya mambo ili baadaye waweze kupandishwa vyeo zaidi kuliko Watanzania wanavyotarajia.”

Akijibu hoja hizo, Jaji mstaafu Nsekela alisema maswali aliyoulizwa siyo ya maadili na angependa ulizwe masuala yanahusu maadili. “Jambo la kwanza lazima uangalie sheria inasemaje. Waheshimiwa wabunge tunapozungumzia maadili ni lazima mpate sheria mliyoitunga inasema nini, nadhani kwa hilo nimeeleweka.

Hata alilouliza Ally Kessy alihoji waliorudisha fedha sijui ni kina nani hao ila tuje kwenye jambo la msingi hilo jambo lipo katika Sheria ya Maadili na sisi tunashughulikia maadili siwezi kwenda katika jambo alinihusu kwa hiyo wabunge mnielewe,” alifafanua.

“Maadili ninayoyazungumzia mimi ni ya sheria ya mwaka 1995 kama ilivyorekebishwa mara mbili inawezekana kuna maovu yanatendeka, lakini je hayo yapo katika sheria yangu. Maadili yanayozungumziwa ni yale ambayo yapo katika sheria, mfano sheria ya rushwa hiyo haipo kwangu ndio maana adhabu zangu ni kuteremshwa cheo, kujiuzulu.”