Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 12:51 pm

NEWS: NDUGULILE AKITAKA CHUO CHA MUHIMBILI KUTOA TAFITI KWA LUGHA NYEPESI

Dar es Salaam: Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amekitaka Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi na Afya Muhimbili (Muhas) kutumia tafiti zinazofanywa chuoni hapo katika kuisaidia Serikali kutimiza majukumu yake kwa kuwasilisha tamko la kisera mara baada ya kuzitangaza.

Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 26, 2018 alipokuwa akizindua kongamano linalohusisha zaidi ya tafiti 21 za watu walioathirika na dawa za kulevya zilizofanywa na chuo hicho.

Dkt. Ndugulile amekitaka chuo hicho kutoa tafiti zao kwa lugha nyepesi huku wakiishirikisha Serikali ili kuendana na kipaumbele kama taifa na kuhakikisha wanatengeneza matamko kisera.

“Tunachoangalia ni namna gani tunaweza kuwasaidia watu wanaotumia dawa za kulevya, mwelekeo tulionao awamu hii ya tano ni kutengeneza sera, uamuzi na uendeshaji unaozingatia takwimu zilizopo na tunawaangalia ninyi kama wazalishaji wakubwa wa takwimu,” amesema Dk Ndugulile.

Amesema Serikali inategemea takwimu kutoka kwa wanasayansi watafiti lakini kumekuwa na upungufu mkubwa katika hilo.

“Tangu niwe Naibu Waziri yapata miezi 10 sasa, sijaona tafiti zenu mkizitengeneza kwa lugha nyepesi ili imsaidie yule mwananchi wa kawaida, haina maana sana kama tafiti zenu zikachapishwa katika majarida makubwa duniani lakini usiisaidie nchi.”

“Kuanzisha utoaji wa tafiti hizi ninaona ni mwanzo mzuri, nitoe rai kwa vyuo vingine vikuu kuwa chimbuko la tafiti na takwimu ili kuboresha sera,” amesema.

“Tafiti zenu ziwe maeneo ya kipaumbele na sisi tufanyie kazi msifanye tafiti kwa sababu mmepata fedha, bali zitakazosaidia jamii, tunatarajia mtafanya tafiti zenye kuleta maana na kuisaidia Serikali kiutendaji.