Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 6:45 pm

NEWS: NDALICHAKO ATOA ONYO KALI KWA TAASISI ZA UMMA ZINAZOJENGA MADARASA YA CHUO CHA AFYA.

DAR ES SALAAM: Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameitahadharisha taasisi ya umma iliyokabidhiwa dhamana ya kujenga madarasa ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kampasi ya Mloganzila kutomwangusha Rais Magufuli.


Ndalichako ametoa tahadhari hiyo baada ya kutembelea mradi huo wa ujenzi wa madarasa kwenye Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Muhimbili tawi la Mloganzila na kukuta ujenzi haujaanza wakati tayari ameshatoa fedha zaidi ya bilioni tatu kwaajili ya ujenzi huo.

“Kifusi kinaanza kuja lini? Maana nimetoa fedha bilioni 3 na milioni 939 tangu Agosti 16, 2017 ili ujenzi ukamilike kuondoa changamoto ya udahili katika fani ya afya, lakini hakuna kilichofanyika hadi sasa, hata matofali ya kujengea hakuna, sasa kazi kwenu nyie ni taasisi ya afya kama mmeamua kumwangusha Rais wenu mimi siwezi kuwasemea”, amesema Ndalichako wakati akiongea na msimamizi wa mradi huo.

Aidha Waziri Ndalichako amemweleza msimamizi huyo kuwa lazima wajiandae kukamilisha ujenzi huo kabla ya mvua za Masika kuanza kwasababu zitakuwa kisingizio cha ujenzi kusimama.

Novemba 25 mwaka huu, Rais Magufuli alifungua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kampasi ya Mloganzila ambayo pia itatumika kama kituo cha kufundishia kwa wanafunzi wa fani ya Afya baada ya kukamilika kwa ujenzi wa madarasa.