Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:29 pm

NEWS: NDALICHAKO ALILIA AJIRA KWA VIJANA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema kutokana na ongezeko la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana nchini, kuna umuhimu wa kutengeneza mazingira kwa ukuaji wa biashara ili ajira nyingi zipatikane kiurahisi kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu ili waweze kujiajiri.

Waziri huyo amebainisha jana Dar es Salaam kuwa kwa sasa Tanzania ina vijana wengi wenye umri wa miaka 15 hadi 34 ambao hawana ajira kutokana na kukosa ujuzi wa kupata ajira ambapo tatizo hilo kwenye miji mikubwa limefikia asilimia 22.3 ikilinganishwa na vijijini ambako ni asilimia 7.1. Alisema hayo wakati akizungumza katika uzinduzi wa Programu za Benki ya Barclays Tanzania zijulikanazo kama Twende Kazi na Balozi Mwanafunzi jijini Dar es Salaam jana.

Profesa Ndalichako alisema tatizo la ukosefu wa ajira linaongezeka kutokana na kutokuwapo kwa uwiano wa ugavi na mahitaji kwenye soko la ajira pamoja na ongezeko la ajira kubakia kwenye sekta isiyo ya kilimo. “Kila mwaka wasichana na wavulana wanaingia kwenye soko la ajira na wanatokana na wahitimu wa sekondari na elimu ya juu ambao wamehama kutoka vijijini kuja mjini kutafuta ajira,” alisema.

Alisema kiwango hicho cha ukosefu wa ajira nchini kinapimwa na idadi ya watu, vijana wasomi wanaotafuta ajira kama asilimia kubwa ya nguvu kazi hali inayosababisha kuwepo na umuhimu wa kutengeneza mazingira mazuri kwa ukuaji wa biashara nchini ili ajira nyingi zipatikane kwa urahisi. Aliishukuru Benki ya Barclays kwa kuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali na jamii katika kuhakikisha tatizo la ukosefu wa ajira linatatuliwa na kupungua kwa kiwango kikubwa kwa kuwawezesha vijana.

Alisema katika miaka 15 ya uwepo wake sokoni, benki hiyo imechukua hatua kupitia mfumo wake wa Shared Growth unaoenda sambamba na Programu ya Twende Kazi, kuwasaidia wahitimu 200 watakaowekwa katika mafunzo ya kujiandaa na soko la ajira katika kampuni mbalimbali nchini kupitia utendaji kazi wa kampuni isiyo ya kiserikali ya Junior Achievement Tanzania ili kupata walio bora zaidi. Alisema pamoja na kutatua tatizo la ajira, benki hiyo pia imesaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kujikimu na ada na mahitaji ya chuo kupitia Programu ya Balozi Mwanafunzi ambapo wanafunzi 23 wa mwaka wa kwanza hadi wa nne watasomeshwa miaka mitatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).