Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:01 pm

NEWS: NDALICHAKO ALIA NA TAKWIMU POTOFU.

JIJINI DOM: Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia profesa Joyce Ndalichako amewataka wadau wa elimu kufanya mapitio na kujiridhisha kuhusu takwimu wanazotoa ili kuondoa upotoshaji unaofanyika.

Akifungua mkutano wa wadau wa elimu leo kwa ajili ya kufanya mapitio ya utendaji wa sekta hiyo jijini Dodoma profesa Ndalichako amesema hadi kufikia juni 2018 serikali ilishatoa asilimia 86.5 ya bajeti iliyopitishwa kwa mwaka 2017/2018 tofauti na taarifa zilizotolewa kuwa ni asilimia 56 tu ndio iliyotolewa.

Aidha amesema serikali ya awamu ya tano imeweka kipaumbele katika sekta ya elimu na ili kudhihirisha hilo imekuwa ikiongeza bajeti kila mwaka ambapo mwaka 2017/2018 ilitenga kiasi cha shilingi trilioni 1.3 na mwaka 2018/2019 imetenga shilingi trilioni 1.4.

Pia amewataka wadau hao kutumia mkutano huo kuweka mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo ikiwemo uhaba wa walimu na utoro shuleni kwa baadhi ya watu ikiwemo wanaotoka katika jamii ya wafugaji.

Mkutano huo wa siku nne uliobeba kauli mbiu isemayo utoaji wa elimu bora katika uchumi wa viwanda umehusisha wadau mbalimbali wa elimu hapa nchini kwa ajili ya kujadili mafanikio na changamoto na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana nazo.