Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 3:43 am

NEWS: MWENYEKITI MAJULE AWATAKA WANACHAMA KULIPA ADA KWA UHAI WA JUMUIYA.

MPWAPWA DOM: Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake(UWT) mkoa wa Dodoma NEEMA MAJULE ameendelea na ziara yake mkoa wa Dodoma kwa kutembelea kata ya Nghambi na Gulwe zilizopo katika wilaya ya Mpwapwa.

Akiwa katika ziara hiyo amesisitiza suala la uhai wa jumuiya kwa kulipa ada na kuwataka viongozi kutoruhusu mwanachama kuingia kwenye vikao vya jumuiya kama sio mwanachama hai.

Majule alisema uhai wa jumuiya ni wanachama walio hai hivyo iwekwe mikakati itakayosimamiwa ili wanachama wajenge utamaduni wa kulipa ada.

"Viongozi kila kikao mkiingia kagueni kadi mjue je wanaoingia kwenye kikao ni wanachama hai? Kwa kufanya hivyo itasaidia watu kuwa na mwamko wa kulipa ada,"alisema Majule.

Katika kufanikisha suala la kuingiza wanachama wapya Majule alizindua rasmi shindano na kuahidi kutoa zawadi kwa wilaya itakayokuwa ya kwanza kuingiza idadi kubwa ya wanachama.

Ziara hiyo imewashirikisha pia wabunge wa viti maalum Fatma Towfiq,Felister Bura na mjumbe wa baraza kuu la UWT Taifa Chiku Mugo.