Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 4:05 pm

NEWS: MWENYEKITI LAWAMANI KWA KUKATA FEDHA ZA TASAF

DODOMA: Wazee wenye zaidi ya miaka 60 wa kata ya Hombolo Bwawani wamemtupia lawama mwenyekiti wa kata hiyo Livingston Yona kwakuwakata fedha wanazolipwa na mpango wa kusaidia kaya masikini(TASAF).

Wazee hao akiwemo Halima Kondo,Elisha Isaya na Mariam Chinoto walisema wanashangazwa sana na kitendo cha mwenyekiti Huyo kuwalazimisha kuwakata fedha hizo pindi wanapotoka kuzichukua.

Huku wakidai malipo ya fedha hizo kulipiwa bima ya afya ya CHF ilihali serikali imetangaza kutoa huduma ya afya bure kwa wazee.

Aidha walisema inasikitisha kuona mwenyekiti huyo kuwatishia kuwa wasipofanya hivyo majina yao yataondolewa katika awamu ijayo.

Waliongeza kuwa licha ya fedha zao kukatwa kwa ajili ya bima bado wamekuwa wakiambiwa wakanunue dawa kwenye maduka ya dawa binafsi pindi waendapo kutibiwa katika kituo chao cha afya.

‘’kwa sababu hata ukienda hospitalini unadaiwa hela, bima hiyo unakuwa umepata ya bure dawa unaambiwa ukanunue sasa faida iko wapi,’’alisema Chinoto.

Mbali na hayo wazee hao wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati ili kuwasaidia kilio hicho.

‘’Ukifika hospitali unaambiwa kanunue dawa Magufuli sijamsikia hata siku moja akisema wazee watibiwe kwa hela Magufuli aje atuone na siye kilio chetu,’’alisema kondo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Livingston Yona Alikana kuhusika na tuhuma hizo na kuongeza kuwa wazee hutibiwa bure kama sera ya afya inavyoelekeza.

‘’Hapana sisi hatuwakati fedha za Tasaf bali sisi tunawahamasisha wale wazee na wale wote waliopo kwenye mpango wa Tasaf wajiunge kwa sababu kule nyumbani kwao wazee Walio wengi wanawajukuu wanawatoto ambao watakapo pata maradhi watashindwa kuwahudumia,’’ alisema.

Hata hivyoYona alisema mpango wa Tasaf ni kuwasaidi watu kwenye masuala ya elimu,afya pamoja na kujikwamuwa na umasikini.

‘’Kwahiyo sisi tunawahamasisha kwamba wao wajiunge kwenye bima ya afya wao kwa hiyali yao wanaafiki tunakubaliana nao na baadae tunawaonesha wale watu wanatakiwa kukata na wanakata,’’alisema.

Hata hivyo ikumbukwe kuwa serikali kupitia kwa waziri mwenye dhamana ya afya Mh.Ummy Mwalimu siku ya june 04 akiwa Bungeni mjini hapa alizikumbusha halmashauri zote nchini kutoa kadi za matibabu ya bure kwa wazee ili kuwaondolea usumbufu wanaoupata wanapohitaji huduma hiyo