Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:46 pm

NEWS: MWANAFUNZI ALIYEKUTA AMEKUFA AZIKWA UPYA.

KILIMANJARO: Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ameongoza mamia ya wananchi kwenye maziko ya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Scholastica, Humphrey Makundi (16) yaliyofanyika juzi jioni katika Kijiji cha Kwamakundi, Moshi mkoani hapa.

Makundi alipotea Novemba 6, mwaka huu akiwa shuleni na mwili wake kuokotwa katika mto Ghona na kuzikwa katika makaburi ya Karanga, kabla ya kufukuliwa na kuhifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC hadi jana.

Akizungumza katika maziko hayo, Mghwira aliiomba Mahakama na vyombo vya upelelezi vifanye kazi yake kwa makini na kuhakikisha wote waliohusika na tukio hilo wanachukuliwa hatua.

Aidha alisema walikuwa wanaamini shule za binafsi zinalea vizuri watoto kwa sababu zinachukua idadi wanayoweza kuihudumia, lakini tukio hilo linaonesha walimu wamesahau wajibu wao wa kulea watoto wanapokuwa shuleni.

Mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi ) aliwaomba wananchi watulie na kuviacha vyombo vya sheria vifanye kazi yake, pia aliiomba serikali isivumilie udhaifu uliopo kwenye sekta ya elimu hasa shule, ambazo hazina uangalizi mzuri wa watoto.

Akiongoza ibada ya maziko, Askofu Msaidizi wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Samweli Mshana alisema Kilimanjaro ni mkoa wenye amani, lakini watu wachache wanaofanya matukio ya mauaji wanaharibu sifa hiyo na kutaka taasisi zinazohusishwa na matukio hayo zifutwe.

Hivi karibuni watuhumiwa watatu kati ya 11 wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi huyo, walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kusomewa mashitaka ya mauaji.

Washitakiwa wawili, Hamis Chacha aliyekuwa mlinzi wa shule ya Scholastica na Labani Nabiswa walifikishwa mahakamani hapo, wakitokea Kituo Kikuu cha Polisi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi wenye silaha.

Baada ya nusu saa, mmiliki wa shule hiyo ya Scholastica, Edward Shayo alifikishwa mahakamani hapo na askari kanzu akitokea Hospitali ya Rufaa ya KCMC, alipokuwa akipatiwa matibabu ya baada ya kupata tatizo la kiafya tangu kushikiliwa kwake.

Upande wa Jamhuri katika shtaka hilo lililofika mbele ya Hakimu Mkazi, Juliet Mawore uliwakilishwa na Mwanasheria Kassim Nassiri akisaidiana na Wakili wa Kujitegemea Faygrace Sadallah huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Eliakunda Kipoko anayemtetea mshitakiwa wa pili Shayo.

Akisoma maelezo ya hati ya mashtaka mbele ya mahakama hiyo, Nassiri alieleza kuwa Novemba 6, mwaka huu mshitakiwa wa kwanza, Chacha (28), wa pili Shayo (63) na wa tatu Laban (37) walimuua kwa kukusudia mtu aitwaye Humphrey Makundi.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Mawore alieleza kuwa washitakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shitaka la mauaji, huku akiwataka kusubiri kufanya hivyo pindi watakapofikishwa Mahakama Kuu ambapo watapata nafasi ya kuwasilisha mashahidi wao pamoja na kujitetea.

Kuhusu upelelezi wa shtaka hilo, Nassiri aliieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika huku akiwasilisha ombi la kupangwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo wakati upelelezi ukikamilishwa. Hakimu Mkazi Mawore aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 8, mwaka huu na washtakiwa wote walirudishwa rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, zikiwa zimepita siku 11 tangu kufukuliwa kwa mwili wa mtu aliyezikwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kuondoa utata wa kupotea kwa mwanafunzi Humphrey, aliyekuwa anasoma shule ya sekondari ya Scolastica iliyopo mji mdogo wa Himo mkoani Kilimanjaro.