Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 5:34 am

NEWS: MWALIKO WA RAIS MAGUFULI WAKWAMISHA KESI YA KINAMALINZI

Dar es Salaam: Kesi inayomkabili aliykuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wa wanne ya utakatishaji wa Fedha na kughushi Nyaraka imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mashahidi kuitwa Ikulu na Rais John Magufuli Jana Octoba 19, 2018 kwaminajili ya kuipongeza Timu ya " Taifa Taifa staa"

Jana Ikulu jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alikutana na kula nao chakula cha Mchana viongozi wa TFF na baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania 'taifa staa'

Kauli hiyo imeelezwa leo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati wa kesi hilo ilipotajwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi upande wa Jamhuri.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa mashtaka ya utakatishaji wa fedha ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana, huku wenzao Zayumba na Frola wakiwa nje kwa dhamana.

Oktoba 16 kesi hiyo iliahirishwa baada ya wakili Kimaro kuiomba mahakama impe muda apitie mwenendo wa kesi kwa sababu ilikuwa inaendeshwa na wakili mwingine wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kimaro amedai mashahidi ambao alikuwa anawategemea kufika kwa ajili ya kutoa ushahidi wameitwa Ikulu.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji na mashahidi ambao tulisha waandaa wameitwa na Rais Magufuli Ikulu hivyo tunaomba tarehe nyingine ili tuweze kuendelea," ameeleza Kimaro.

Upande wa mashtaka baada ya kuwasilisha hoja hizo, wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza alilalamika kwamba hoja ambazo zimetolewa na wakili Kimaro zinaonyesha ni dharau kwa sababu kesi hiyo ina mashahidi wengi ambao sio wote waliitwa Ikulu.

"Naomba upande wa mashitaka wajitahidi kutuletea mashahidi wa kutosha ili kesi iweze kuendelea kuliko kusubiri mashahidi hao tu,” alisema.

Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, aliuagiza upande wa mashitaka kupeleka mashahidi wa kutosha Oktoba 30 na Novemba Mosi kesi hiyo itakapoendelea na usikilizwaji ushahidi .

Mbali na Malinzi, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga.

Wengine ni meneja wa ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na karani wa shirikisho hilo, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha dola za Marekani 173,335 na Sh43,100,000.