Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 6:51 am

NEWS: MTATURU AWAPA NEEMA WAKAZI WA KIMBWI IKUNGI.

IKUNGI SINGIDA: Mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu ameruhusu kuanza rasmi shughuli za uvuvi katika bwawa la Muyanji lililopo katika kijiji cha Kimbwi alilolifunga kwa takribani miezi sita ili vifaranga vya samaki vilivyopandikizwa viweze kukua.

Vifaranga hivyo vilipandikizwa mwishoni mwa mwezi february 2018 ili vikue.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kimbwi akiwa katika ziara kwenye bwawa hilo ambalo linaajiri wavuvi zaidi ya 3,000 wanaofanya shughuli mbalimbali za kiuchumi Mtaturu amesema dhamira ya serikali ya kuzuia uvuvi kwenye bwawa hilo ilikuwa kuhakikisha wanaboresha mazingira ili wavuvi wafanye kazi vizuri na maisha ya watu yaweze kuboreshwa.

“Mwaka jana nilimuagiza mkurugenzi wa halmashauri aafunge bwawa hili ili tupandikize vifaranga wakue vizuri ndipo tuanze kuvua,niwashukuru viongozi wa kijiji kwa kusimamia agizo hili la serikali na kwa wavuvi nyinyi wenyewe kwa kuwa wavumilivu na kutii maelekezo yetu,ahsanteni sana,”alisema Mtaturu.

Amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri Rustika Turuka na katibu tawala wa wilaya Winifrida Funto kuhakikisha katika maombi ya watumishi waombe waletewe afisa uvuvi wilaya ili asaidie kuelimisha namna bora ya kuvua.

“Kipindi hiki ambapo mchakato unaendelea hakikisheni mnamuomba afisa uvuvi mkoa ilia je awaelimishe na kuwaongoza katika kuzingatia kanuni za uvuvi,”aliongeza Mtaturu.

Amewaasa wavuvi hao kuzingatia kuvua samaki kwa kutumia nyavu ya nchi tatu ili kutoruhusu samaki wachanga kuvuliwa na hivyo kupelekea kupoteza mbegu iliyopandwa katika bwawa hilo.

Aidha Mtaturu amewataka kila mmoja kuwa mlinzi wa bwawa hilo na kendesha shughuli ya uvuvi kwenye vikundi ili kuwezesha kumtambua mgeni atakayekuja kutoka sehemu nyingine na kuvua bila ya kufuata utaratibu.

Akizungumza mkazi mmoja wa kijiji hicho Abdallah Alli ambaye ni mvuvi tangu mwaka 1984 amemshukuru mkuu wa wilaya hiyo kwa kuwa msaada kwao.

“Bwawa hili kwa muda mrefu tulikuwa tunalihangaikia sana bila ya msaada wowote,lakini wewe umekuja umetusaidia kutupa nguvu,ndio maana hata ulipolifunga na kutuambia tusivue tulitii na kuwa walinzi bila ya malipo yoyote,tunakushukuru sana,”alisema mzee huyo.

Februari 27 mwaka huu katika zoezi la upandaji miti kiwilaya Mtaturu aliwakumbusha wananchi kufuata kanuni za uhifadhi wa mabwawa kwa kutofanya shughuli za kilimo na ufugaji mita 60 pembezoni mwa bwawa na kuainisha mpango wa halmashauri wa baadae wa kuongeza kina na kutenga bajeti katika mwaka wa fedha wa 2018/2019.