Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 9:45 am

NEWS: MOROGORO YAANZA KUONGOZWA NA TAA ZA BARABARANI

Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) katika kikosi cha Umeme, kimefanikisha mradi wa kufunga taa za kuongozea magari (Traffic lights) katika Manispaa ya Morogoro. Taa hizo za kisasa ambazo zinatumia nishati ya jua zimesimikwa katika makutano ya barabara ya Mei mosi na Korogwe inayotokea kituo kikubwa cha mabasi cha Msamvu kuingia mjini.

Akizungumza wakati wa tukio la usimikaji wa taa hizo, Kaimu meneja wa Kikosi cha Umeme kutoka wakala huo Mhandisi Pongeza Semakuwa alisema mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni mia moja na sitini na sita na ni wa kwanza kufanywa na wakala katika manispaa hiyo, β€˜β€™taa hizi ni za kisasa zaidi na zinatoa suluhisho la muda kwa watumiaji kwakua zinahesabu sekunde mtumiaji akiwa anaona, tupo kwenye majadiliano na TARURA na kuna uwezekano tukasimika taa katika maeneo mengine hapa,’’ alisema Mhandisi Pongeza.

Aidha Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Manispaa ya Morogoro Mhandisi Mnene James amesema wataendesha mafunzo wakishirikiana na TEMESA kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara hizo kuhusu namna sahihi ya kutumia taa hizo na alama za kivuko cha waenda kwa miguu ili kuepusha ajali ambazo zimekua zikitokea mara kwa mara katika eneo hilo hasa kwa madereva wa bodaboda.

Kukamilika kwa mradi huo kunaifanya Manispaa ya Morogoro kuwa na makutano ya pili kuwekwa taa za kuongozea magari baada ya makutano ya barabara ya Mazimbu na Iringa eneo la Tumbaku kupitiwa na mradi kama huo hivi karibuni.