Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:44 pm

NEWS: MMILIKI WA MABASI YA MURO AHUKUMIWA MIAKA 8 JELA AU FAINI 115M

Dar es Salaam: Mmiliki wa Kampuni ya mabasi ya Princes Muro, Majid Kimaro amehukumiwa kifungu cha miaka 8 kwenda Jela au kulipa faini ya Sh115milionil.

Hukumu hii imekuja baada ya mmiliki huyo kukiri mbele ya mahakama shtaka la kutakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu ili kuiba mafuta katika bomba linalomilikiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Kimaro anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuongoza genge la uhalifu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 81/2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Pia, mahakama hiyo imeamuru gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 856 ADH ambalo lilitumika kuiba mafuta zaidi ya lita 26,875.25 ya dizeli na petroli litaifishwe na kuwa mali ya Serikali.


Hukumu hiyo imetolewa leo mchana Jumatano Desemba 12, 2018 na hadi saa 9:40 alasiri mshtakiwa huyo bado alikuwa mahakamani hapo ikielezwa kuwa anafanya taratibu za kulipa faini hiyo.

Akitoa hukumu hiyo Jumatano Desemba 12, 2018 Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema kuwa mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kwa makosa mawili baada ya kukiri.

Simba amesema katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, Muro anapaswa kulipa faini ya Sh5milioni au kifungo cha miaka mitatu jela.

Katika shtaka la utakatishaji fedha mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh110milioni au kifungo cha miaka mitano jela.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, wakili wa Serikali Simon Wankyo akisaidiana na Jacqueline Nyantori na Patrick Mwita wameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa kwa sababu makosa hayo ya wizi husababisha kuathirika kwa uchumi na nchi kukosa mapato.

Pia ameomba gari hilo litaifishwe na kuwa mali ya Serikali kwa sababu ndio lililotumika kubeba mafuta baada ya kulitoboa bomba na kuiba mafuta hayo.


Wankyo amedai katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Julai Mosi, 2016 na Januari 8, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam na maeneo mengine akiwa pamoja na wenzake ambao hawako mahakamani, kwa kujua aliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kutoboa bomba la mafuta la TPA na kuiba mafuta ili kupata faida.

Katika shtaka la pili inadiawa kati ya Julai Mosi, 2016 na Januari 8, 2018 walipata lita 15,950.3 za mafuta ya dizeli na lita 10,925.22 za petroli na kusambaza mafuta hayo kwenye vituo vyake vya mafuta ma kuyauza wakati akijua yametokana na makosa ya uhalifu.