Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:41 am

NEWS: MKURUGENZI MGANGA ''TUNAFANYAKAZI KWA KUZINGATIA KATIBA NA SHERIA''


Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) inafanya kazi kwa kufuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 8 cha Sheria ya Taifa ya Mashtaka Sura ya 430 na kuzingatia nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma na sio kwa kushinikizwa au kwa kuwalinda watumishi au makampuni.


DPP Mganga amesema hayo jijini Dodoma alipokutana na waandishi wa habari kufafaunua juu ya taarifa zinazosambazwa na wamiliki wa makampuni hayo juu ya kufikishwa Mahakamani kwa watumishi wao na kampuni zao za Pangea Minerals Limited, North Mara Gold Mine Limited, Exploration Minerals Du Nord LTEE na Bulyanhulu Gold Mine Limited kuwa kunatokana na shinikizo la Serikali.


“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) inafanya kazi kwa kufuata matakwa ya Ibara ya 59B (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 8 cha Sheria ya Taifa ya Mashtaka Sura ya 430 huku tukizingatia nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma; kwa msingi huo hatufanyi kazi zetu kwa mashinikizo au kwa kuwawinda watumishi au kampuni fulani,” amesema DPP.


Amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) hutekeleza majukumu yake kwa kutegemea uhusika wa watuhumiwa katika vitendo vya jinai na kufafanua kuwa kufikishwa Mahakamani kwa watumishi hao na kampuni zao kunatokana na kuridhishwa na ushahidi uliopatikana na mabao unaonesha matendo ya kijinai ya watumishi hao kwa nafasi zao ndani ya makampuni hayo kwa nyakati zilizotajwa kwenye hati ya mashtaka na ushiriki wa makampuni hayo kwa wakati huo ambapo uchunguzi umebaini kuwa walivunja sheria.


Amesema upelelezi unaondelea ndio kigezo kikuu kinachotumiwa na NPS kufungua kesi ya jinai na kuongeza kuwa katika kesi hiyo idadi ya washtakiwa, aina ya mashtaka na kiasi cha fedha kilichohusika vitaendelea kubadilika kwa kadiri upelelezi juu ya masuala hayo utakavyokuwa unaendelea na kukamilika.


“Ieleweke wazi kwamba katika kesi zilizofunguliwa idadi ya washtakiwa, aina ya mashtaka na kiasi cha fedha kilichohusika vitaendelea kubadilika kwa kadiri upelelezi juu ya masuala hayo utakavyokuwa unaendelea na kukamilika; upelelezi unaondelea ndio kigezo kikuu kinachotumiwa na Ofisi yetu kufungua kesi ya jinai,” alisisitiza DPP.


Amesema hii sio mara ya kwanza kwa watumishi na makampuni yao kushtakiwa mahakamani kwani wapo baadhi ya watumishi na makampuni yao kesi zipo mhakaman na nyingine zimeisha kwa watumishi na makampuni yao kutiwa hatiani na kuadhibiwa.


DPP Mganga pia ameeleza kuwa kesi ilizofunguliwa dhidi ya watumishi hao na makampuni yao hazihusiani na shauri au mashauri yaliyofunguliwa katika Baraza la Usuluhishi na makampuni yay a Bulyanhulu na Buzwagi na kwamba kuwepo kwa mashauri hayo katika baraza hilo la usuluhishi hakuizuii NPS kufungua shauri la jinai kwa mtu au kampuni


DPP Mganga amewataka wananchi na wawekezaji kutekeleza majukumu yao bila hofu au mashaka kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi ya amani inayofuata misingi ya utawala wa sheria na kuzingatia Katiba ya nchi.


Oktoba 17 na 23 2018, Watumishi watatu akiwamo mmoja mstaafu pamoja na kampuni nne za Pangea Minerals Limited, North Mara Gold Mine Limited, Exploration Minerals Du Nord LTEE na Bulyanhulu Gold Mine Limited nayo pia walifikishwa Mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 39 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kukwepaji kodi, kutakatisha fedha, kutoa msaada kusimamia mkakati wa kihalifu kwa ajili ya kupata faida, rushwa na kuongoza kutendeka kwa uhalifu.


Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama waliyopelekwa haina uwezo wa kusikiliza mashtaka hayo na walipelekwa rumande hadi Oktoba 31 ambapo kesi hiyo itakapotajwa tena.