Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:38 am

NEWS: MIMBA ZAKATISHA NDOTO ZA WASICHANA 150.

KONGWA DODOMA: Wasichana 150 katika wilaya ya Kongwa walikatisha masomo kutokana na ujauzito kwa kipindi cha miaka minne.

Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu katika wilaya ya Kongwa Selina Fundi amesema hayo jana kwenye ufunguzi wa klabu za msichana amani kwenye Shule ya Sekondari ya Sejeli kwenye mradi unaotekelezwa na Shirika la Msichana Initiative (MI) chini ya ufadhili wa ubalozi wa Ufaransa kupitia mradi wa DEFI wenye lengo la kupinga ukatili wa kijinsia.

Amesema mila na desturi zimekuwa chanzo kikubwa cha wasichana kukatisha masomo.

“Mara nyingi mtoto anapovunja ungo wazazi wanaona ni bora aolewe na haina haja tena ya kuendelea na masomo” amesema

Alisema umbali mrefu kutoka makazi wanayoishi wanafunzi wengi imekuwa ni miongoni mwa vyanzo vya wanafunzi kujiingiza kwenye ngono.

“Wanafunzi wanatembea zaidi ya kilomita 10 kufika shuleni na huku anakutana na watu wanaoweza kumpa msaada”

Amesema katika kipindi cha miaka minne jumla ya wanafunzi 150 walikatisha masomo kutokana na ujauzito ambapo mwaka 2015 waliokatisha masomo walikuwa 27, mwaka 2016 walikuwa wanafunzi 30, mwaka 2017 wanafunzi 48na mwaka huu mpaka sasa jumla ya wanafunzi 45 wameshapata ujauzito.

“Tunahitaji kusaidia wasichana ili waweze kutimiza ndoto zao, mkakati wa muda mrefu uliopo ni kuhakikisha shule za sekondari zinapata hostelikwani umbali kutoka makazi ya wanafunzi ni changamoto kubwa kwani sit u wasichana wanapata mimba hadi watoto wa kiume wanaamua kuacha shule” amesema

Amesema baadhi ya kesi ziko polisi na nyingine mahakamani na changamoto kubwa ni wazazi wanaamua kumalizana wenyewe kwa wenyewe na wamekuwa hawatoi ushirikiano kesi zinapofikishwa polisi hali inayochangia kesi hizo kushindwa kuendelea.

Ofisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Kongwa, Jovita Mamku alisema mila na desturi kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikichangia kuongezeka kwa mimbana ndoa za utotoni katika wilaya hiyo.

Amesema jamii bado inahitaji kuelimishwa ili ifahamu haki za mtoto wa kike na iweze kuwasaidia ili watoto watimize ndoto zao.

“Elimu inaendelea kutolewa katika jamii ili kuweza kupinga masuala ya ukatili na mimba na ndoa za utotoni” amesema

Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Sejeli, Winfrida Mtagwa alisema mimba zina hasara kubwa kwa wasichana katika maisha yao ya baadate.

Meneja Mradi wa Shirika la Msichana Initiative Lineth Masala amesema kwa muda wa wiki mbili na nusu wamekuwa mkoani Dodoma, wilaya ya Chamwino na Kongwa wakifungua klabu 22 za msichana na amani zinazowakutanisha watoto wa kike na wa kiume ambapo shule 11 ni katika wilaya ya Chamwino na shule 11 katika wilaya ya Kongwa.

Amesema lengo la klabu ni kuelimisha ni kuelimisha watoto juu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni, elimu ya afya ya uzazi, kujiamini na kujitambua na klabu hizo zinawapa wanafunzi nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu haki zao na kujua namna ya kupaza sauti zao.