Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 5:42 am

NEWS: MIFUGO ISIYO NA CHAPA KUKAMATWA.

TABORA: Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, Abel Busalama ameagiza kukamatwa mifugo yote itakayokutwa wilayani humo bila kuwa na chapa ya utambulisho baada ya kufungwa utaratibu wa upigaji chapa.

Busalama alitoa agizo hilo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Zugimlole wilayani humo ambapo alisema serikali inatambua umuhimu wa mifugo na wafugaji na imedhamiria kuboresha miundombinu yote ya mifugo na kuhamasisha ufugaji wa kisasa.

Alisema halmashauri ya wilaya hiyo inajivunia kuwa na mifugo mingi katika mkoa huo kwani imeweza kuchochea ongezeko kubwa la mapato ya ndani na kwamba mwaka jana pekee makusanyo yaliyopatikana kutokana na mifugo ni zaidi ya Sh milioni 80.

Alibainisha kuwa sekta ya mifugo ni ya pili kwa kuzalisha mapato mengi ya halmashauri hiyo ikiwa nyuma ya sekta ya kilimo, hivyo inapaswa kupewa kipaumbele kwa kuboresha miundombinu iliyopo ya malisho, majosho, malambo bila kusahau afya za mifugo hiyo.

Busalama alisisitiza haja ya kutambua idadi halisi ya mifugo yote iliyoko katika wilaya hiyo kupitia utaratibu wa upigaji chapa na kwamba atakayekaidi agizo hilo akamatwe yeye na mifugo yake ili achukuliwe hatua za kisheria.

Aidha alifafanua kuwa utaratibu wa upigaji chapa ni wa kimataifa na yeyote atakayebakia au atakayepitishwa katika wilaya hiyo na wafanyabiashara bila kuwa na chapa ya utambulisho wa eneo alikotoka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dk John Pima alisema halmashauri yake imejipanga vizuri kuboresha mifugo na ufugaji ikiwemo kupata kilo nyingi za nyama na maziwa.

Ofisa Tawala wa Wilaya hiyo, Michael Nyahinga alimhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa atafuatilia na kusimamia utekelezaji wa maagizo yote aliyotoa, ikiwemo kukamatwa kwa mifugo yote itakayoingizwa wilayani humo bila kuwa na chapa ya utambulisho Hata hivyo, alimtaka mkurugenzi wa halmashauri kuboresha na kuimarisha usimamizi wa mifugo na minada iliyopo katika wilaya hiyo ili kuongeza thamani ya mifugo na kuwezesha ukusanyaji wa mapato mengi zaidi yatokanayo na mifugo