Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 3:44 am

NEWS: MFANYABIASHARA NGULI WA MADAWA YA KULEVYA AKAMATWA NA MKE WAKE

Dar es Salaam: Kamishna wa Operation Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Fredirick Milanzi amesema amemkamata mtuhumiwa wa biashara ya mihadarati, Ayoub Kiboko nyumbani kwake jijini Dar es salaam.

Milanzi alisema kuwa walimkamata kiboko akiwa na dawa za kulevya aina ya Heroin gram 250 kwenye msako wa usiku wa manane nyumbani kwake

“Baada ya kumkamata mtuhumiwa akiwa na dawa hizo tulitumia vifaa vyetu kupima dawa hizo na tuligungua ni heroin. Lakini anayestahili kutoa majibu ni mkemia mkuu wa Serikali hivyo tumeshapeleka sampuli kwa ajili ya uthibitisho tunasubiri ili ikithibitika mtuhumiwa afikishwe mahakamani,” alisema Milanzi. Akisimulia namna walivyomkamata Kiboko, Milanzi alisema walipofika katika jumba la kifahari la ghorofa mbili la mtuhumiwa huyo huko Tegeta, waliomba kumkagua lakini alikataa. “Hata hivyo, maofisa wetu walitumia mbinu zao na kufanikiwa kumkagua kisha kubaini dawa hizo,” alisema.

Alisema katika upekuzi huo walimkuta Kiboko akiwa na bastola ya kichina. “Lakini tulipoikagua tulibaini anaimiliki bastola hiyo kihalali. Tulimkuta na unga mwingine ambao hatuwezi kutaja ni kiasi gani au ni wa aina gani mpaka utakapopimwa na mkemia mkuu wa Serikali,” alisema Katika ukaguzi huo,

Kiboko ambaye ni mfanyabiashara maarufu ndani na nje ya nchi anadaiwa kumiliki hoteli kubwa zaidi ya 10 pamoja nyumba za kifahari katika maeneo mbalimbali hapa jijini. Mtuhumiwa huyo ambaye DCEA imesema ilikuwa ikimsaka kwa muda mrefu, alikamatwa pamoja na mkewe Pilli Kiboko Mei 23 saa 8 usiku wakiwa nyumbani kwao eneo la Tegeta. Kiboko ni miongoni mwa wafanyabiashara waliotajwa katika barua za Watanzania waliofungwa Hong Kong.

Barua hizo zililetwa nchini Desemba 2014 na Kasisi John Wotherspoon anayesaidia wafungwa katika magereza ya Hong Kong na China. Watanzania hao waliandika barua hizo wakiwaasa wengine wasifanye biashara hiyo huku wakiwataja wafanyabiashara waliowabebesha dawa hizo za kulevya akiwamo Kiboko.

Milanzi alisema walipofika kwake walikamata baadhi ya mali za Kiboko yakiwamo magari yake matatu. Milanzi alidai kuwa mtuhumiwa huyo alianza biashara hiyo muda mrefu na taarifa zinaonyesha kwamba huwatumia vijana mbalimbali kupeleka China. “Baadhi ya vijana waliohukumiwa kunyongwa China, walimtaja yeye (Kiboko) kuwa ndiye huwatuma,” alisema.