- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MBOWE ALALA TENA SEGEREA
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wamerudishwa gereza la Segerea baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusimamisha usikilizaji wa rufaa yao hadi pale rufaa ya Serikali itakapoamuriwa.
Serikali imekata rufaa Mahakama ya rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kuu kusikiliza rufaa ya wawili waliyoiwasilisha mahakamani hapo kupinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 23, 2018.
Baada ya uamuzi wa Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza rufani hiyo ya Mbowe na Matiko kutoa uamuzi huo leo jioni Ijumaa Novemba 30, 2018 Mbowe aliwasalimia wafuasi wa chama chake waliofurika mahakamani hapo kuwa ‘People’s nao wakaitikia Power.”
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania alimalizia kwa kuwaeleza, ‘mapambano yanaendelea.”
Jaji Rumanyika amefikia uamuzi huo wa kusimamisha usikilizaji kufuatia uamuzi wa upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili washtakiwa hao kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Jaji Rumanyika amekubaliana na hoja za Serikali kuwa uamuzi mdogo hauwezi kumaliza shauri hauwezi kukatiwa rufaa na wadaiwa wengine isipokuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) tu.
Jaji Rumanyika amesema DPP anapewa mamlaka ya kukata rufaa kwa uamuzi mdogo chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa.
Kuhusu taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, amesema hilo liko wazi kwamba kunapokuwepo na taarifa hiyo mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri.
"Hivyo mwenendo wa shauri hili unasimama hadi rufaa iliyokatwa Mahakama ya Rufani itakapoamriwa," amesema Jaji Rumanyika.
Serikali imekata rufaa katika Mahakama ya Rufani, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kukubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya kina Mbowe.
Wawili hao walifutiwa dhamana hiyo Novemba 23, na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, kufuatia maombi ya upande wa mashtaka, kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kutokufika mahakamani tarehe ambazo kesi yao ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Baada ya kufutiwa dhamana hiyo walikata rufaa Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huo wa kufutiwa dhamana.
Kabla ya rufaa hiyo kusikilizwa Serikali iliweka pingamizi la awali ikiomba mahakama iitupilie mbali rufaa hiyo, ikidai ina kasoro za kisheria.
Mahakama Kuu licha ya kukubaliana na baadhi ya hoja za pingamizi la Serikali lakini imezikataa hoja nyingine ambazo zingeweza kusababisha rufaa hiyo kutupiliwa mbali kama ingezikubali.
Hivyo ikaamua kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo.
Hata hivyo, muda wa usikilizwaji wa rufaa hiyo ulipofika ndipo mawakili wa Serikali wakaiarifu mahakama wamewasikisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu.
Mawakili wa Serikali Wakuu, Paul Kadushi na Faraja Nchimbi wamedai mahakama hapo haina mamlaka tena ya kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo ya kina Mbowe kwa kuwa tayari wameshakata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kukubali kuisikiliza rufaa hiyo.
Baada ya taarifa hiyo Jaji Rumanyika amewataka mawakili wa pande zote pamoja na mambo mengine waieleze Mahakama iwapo uamuzi wake huo ambao ni uamuzi mdogo usiomaliza shauri unaweza kukatiwa rufaa.
Upande wa Serikali umesema DPP ana mamlaka ya kukata rufaa hata kwa uamuzi mdogo usiomaliza kesi na ukawasilisha kesi mbalimbali zilizokwisha kuamuriwa na Mahakama ya Rufani kuhusu hoja hiyo.
Mawakili wa kina Mbowe, Peter Kibatala na Jeremia Mtobesya wakijibu hoja za Serikali kwamba baada ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu haina uwezo wa kuendelea na rufaa ya kina Mbowe, wamedai Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo
Hivyo, wameiomba Mahakama Kuu iendelee na usikilizaji wa rufaa hiyo ya wateja wao kama ambavyo ilikuwa imepanga, ili haki ya wateja wao itendeke.